Na John Walter-Babati

Madiwani wa Babati Vijijini wamelitaka shirika la Umeme (TANESCO) kupeleka Umeme maeneo ambayo bado hayajapata huduma hiyo.

Aidha Baraza maalum la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Babati limeomba shirika hilo lipeleke umeme katika taasisi zote za serikali ambazo bado hazijafikiwa.

Wametoa agizo hilo leo katika Baraza maalum la madiwani lililoitishwa kwa lengo la kupata majibu juu ya maswali yanayoulizwa na Wananchi kuhusu upatikanaji wa Maji, Umeme na Barabara katika maeneo yao.

Taasisi zilizoitwa na mkuu wa wilaya ya Babati ya Lazaro Twange kwenye baraza hilo ni TARURA, RUWASA, na TANESCO.

Mwenyekiti wa Baraza hilo  John Noya amesema inasikitisha kuona shule za msingi na sekondari na baadhi zikiwa za Bweni hazina umeme na wao Madiwani wakifuatilia TANESCO hawapewi majibu ya kuridhisha.

Noya ambaye ni Diwani wa kata ya Madunga amesema baadhi ya watendaji wa taasisi hata Simu hawapokei.

Diwani wa Kata ya Kiru Keremu Benjamin  amesema baadhi ya  barabara zilizochongwa na TARURA bila kuwekwa makinga maji zimeshaharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha hivyo Wananchi wanakosa huduma na Serikali kupata hasara.

Diwani wa kata ya Ayasanda Yahaya Hamis amesema Wananchi wanataka huduma na sio maneno hivyo Wataalamu wazungumze ukweli ili wanapokuwa kwenye vikao na Wananchi waeleze 

Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini Daniel Sillo amezitaka taasisi za serikali kushirikisha viongozi wa eneo husika wanapotekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo na kuisimamia kulingana na thamani ya fedha.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro Twange amewataka watendaji wa serikali kufanya kazi kwa bidii na hayupo tayari kumtetea mfanyakazi mzembe.

Meneja wa TANESCO mkoa wa Manyara Mhandisi Jahulula Jahulula amesema katika Mkoa wa Manyara bajeti iliyopita kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya umeme ni Bilioni 2  ambayo haiwezi kukidhi haja.

Kwa upande wake Meneja wa TARURA mkoa wa Manyara amesema amepokea maoni na ushauri wa madiwani na kwamba wanakwenda kuyafanyia kazi. 

Share To:

Post A Comment: