Na Imma Msumba ; Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella amempa mwezi mmoja Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Mhandisi Juma Hamsini kulipa malimbikizo ya posho za wenyeviti wa serikali za mitaa yote 154 katika Halmashauri ya Jiji hilo

Rc Mongella ametoa agizo hilo wakati akiendelea na ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kujengwa katika Jiji la Arusha.

Amesema wenyeviti hao wanapaswa kulipwa fedha zao kila mwezi na amepata malalamiko ya kutolipwa fedha hizo kutoka kwa wenyeviti hao na kusisitiza walipwe fedha zao zote wanazodai kwani ni watu muhimu.

Hata hivyo akiwa kwenye ziara hiyo Rc Mongela ameonyesha kukerwa na uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kushindwa kufikia asilimia 25 ya ukusanyaji wa mapato kwa kipindi cha robo ya mwaka wa fedha wa 2023/24 licha ya kuwa na vyanzo vingi vya mapato. 

Sambamba na hilo Rc Mongela ameagiza miradi yote ya ujenzi inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo kukamilika kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa na pia akisisitiza ni marufuku kuongeza fedha zozote za mapato ya ndani kwa ajili ya kukamilisha miradi ambayo ilishatengewa fedha kwa ajili ya utekelezaji.

Pia amesisitiza Jiji hilo kuwekwa taa za barabarani ili kuwezesha wananchi kupata mwanga nyakati za usiku kwani Jiji hilo ni kubwa katika utalii kupitia filamu ya Royal Tour.

"Arusha ndio kitovu Cha taasisi za Afrika za kisheria na ni Jiji la Utalii hivyo lazima kuwepo na taa lakini pia kuongeza juhudi zaidi katika ukusanyaji wa mapato"

Rc Mongella ametoa maagizo hayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika Halmashauri ya Jiji la Arusha ya kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kusikiliza kero za wananchi hapo kesho anatarajiwa kuendelea na ziara yake katika Jiji hili la Arusha. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Mhandisi Juma Hamsini  amesema atalipa wenyeviti hao hela zao wanazodai na kusisitiza kuwa Jiji hilo litaendelea kufungwa taa pamoja na CCTV camera katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha usalama.Share To:

Post A Comment: