Na John Walter-Hanang'
Mwenge wa uhuru unaendelea na mbio zake katika mkoa wa Manyara huku ukitarajiwa kufika kilele oktoba 14 katika mji wa Babati ukienda sambamba na wiki ya vijana na kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Katika sherehe hizo, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Samia Suluhu Hassan.
Mwenge huo baada ya kuridhishwa na miradi yote katika halmashauri ya wilaya ya Babati, leo oktoba 10,2023, umetembelea na kuzindua miradi nane ya maendeleo katika kata sita, tarafa tatu za wilaya ya Hanang' yenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 2.
Miradi iliyotembelewa na Mwenge ni wa maji katika kata ya Hidet uliogharimu shilingi milioni 177 utakaowanufaisha zaidi ya wananchi 2,270 uliotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA).
Mradi mwingine ni wa kuwawezesha wakulima kufanya kilimo chenye tija ambapo wakulima 10 wamekabidhiwa matrekta 10 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 570 kutoka kampuni ya ukopeshaji zana za kilimo Pass Leasing.
Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2023 Abdalla Shaib Kaim amekabidhi hundi ya shilingi milioni moja kwa kikundi cha lishe katika shule ya Sekondari ya wasichana Nangwa kwa ajili ya kuendeleza miradi ya lishe shuleni hapo na hundi nyingine ya shilingi milioni mbili akikabidhi kwa shule ya msingi Katesh A inayohudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Aidha pamoja na miradi mingine, mwenge umekagua mradi wa bara bara ya kiwango cha lami Ganana ambapo hadi kukamilika kwake unatarajiwa kutumia zaidi ya shilingi milioni 900.
Kiongozi huyo amempongeza mkuu wa wilaya ya hiyo Janeth Mayanja na wataalamu wengine kwa kusimamia vyema fedha za serikali akisistiza utunzaji wa nyaraka za miradi.
Kauli mbiu ya mbio za Mwenge wa uhuru mwaka 2023 "Tunza Mazingira,Okoa Vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe Hai, kwa Uchumi wa Taifa"
Post A Comment: