KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amesema Chama hakitasita kuwachukulia hatua mawaziri, Wakuu wa Mikoa pamoja na watendaji watakaoshindwa kufanya majukumu yao.

Makonda ameyasema hayo Leo octoba 26 mara baada ya kukabidhiwa Ofisi na kuzungumza na wananchi waliofika kumlaki katika ofisi ndogo za Chama, Lumumba jijini Dar es Salaam.

“Naomba kutuma salamu kwa Mawaziri wote, Wakuu wa Mikoa, watendaji wote pale patakapobainika hawajafanya kazi yao kikamilifu chama hakitasita kuchukua hatua, bahati nzuri tunafahamiana,”amesema.
 
Amesema hatakua tayari kuwa Msemaji wa chama ambacho kimepewa dhamana na wananchi na wanaomsaidia Mwenyekiti wa Chama wanaoshindwa kutekeleza asimame hadharani kusema uongo.
 
“Kila kiongozi wa Serikali atabeba msalama wake mwenyewe, sijahifadhiwa miaka mitatu na miezi mitatu kusema uongo, sijateuliwa na CCM kusema uongo na kiapo chetu kipo wazi fitina, uongo uzushi si sehemu ya CCM,”amesema.
 
Amesema haki huinua taifa, chama kimepewa dhamana na wananchi na chama kuunda serikali hivyo kiongozi yeyote atakayebainika na chama kujiridhisha, kitachukua hatua bila kusubiri.
 
“Taifa hili halina upinzani haina chama cha upinzani, bali ina watoa taarifa waliojikusanya katika jina la vyama.
 
“Ukimuona Tundu Lisu anaongea sio Chama ni mtu tu anatoa taarifa na wakati mwingine taarifa anayoweza kuitoa inawezekana ikatoka kwenye chanzo ambayo si cha ukweli au si cha uhakika,”amesema.
 
Amesema kutokana na kuwa ni mtoa taarifa kazi ya Chama, kusikiliza taarifa zao na kushughulika aliyesababisha taarifa kutoka na kwamba watazifanyia kazi taarifa hizo kwasababu ni chachu ya ujenzi wa maendeleo katika taifa.
 
“Mbowe karuka akasema ya kusema, juzi nimemuona Songwe hana helkopta naomba nawaelekeza wanaoshughulika na vibali mbowe apewe vibali aruke na helkopta na kama hana mafuta, nimezungumza na Samia amesema atamchangia.
 
“Akiruka angani tutamfuata, atapigwa kila kona kwasababu moja tu hoja na uwezo na utekelezaji wa chama cha mapinduzi hauna shaka kama kuna mtu anamcheleweshea mbowe kibali, cha kutumia helkopta nikiwa Msemaji apewe kibali,”amesema.
 
Makonda ameliomba Jeshi la Polisi kutoa vibali vya mikutano wawaachie mikutano ya hadhara na kwamba wasihangaike nao kwasababu safu ya Rais Samia miekamilika.
 
“Rais Samia ameendelea kutoa elimu bure, kujenga barabara, afya, viwanja vya ndege kuthamini na kulinda utu wa mtanzania hatuna sababu ya kutegemea polisi, au kuhusu polisi ndiyo msaada wa CCM hoja tunazo,”amesema.
 
Ameongeza kuwa “Taifa linajengwa na upendo, ukiwa unampenda ndugu yako hutamsema na kumsingizia, ukimpenda mwanachama mwenzako hutamfanyia hila, niwaombe wanachama wa CCM tukajenge upendo katikati yetu,”Makonda.
 
Amesema iwe jua au mvua Chama cha Mapinduzi ndiyo baba lao ambapo akiwa msemaji kwa Chama cha pili kwa ukubwa duniani, Sauti ya wanyonge itasikika.

“Dkt Samia ana R zake nne moja anazungumzia mariodhiano, tangu niteuliwe nimepata nafasi ya kupita kwenye mitandao kusoma baadhi ya maoni ya watu wengi wakihamaki….wanaohamaki wengi wao wanawaza tu Makonda atakwenda kulipa kisasi, wanawaza makonda atakwenda kufanya nini na wengine wakiwataja watu wengine , usiyemtaka kaja, wengine wanasema tumejifunza nini kwenye jambo la Makonda. 
 
“Naomba niseme, mimi sina kisasi kwa mtu yeyote na asiwepo mtu yeyote yule akafikiri lengo langu ni kumkandamiza wakati huu nitajitutumua nitaonesha mabavu dhidi ya wale waliofikiri wamenitenda mabaya la hasha,”amesema.
 
Amesema wanaohisi kwamba kuna jambo halikuwa sawa anaelewa Mungu aliwatumia kumsaidia kumjua Mungu zaidi, kumfanya kuwa mnyenyekevu na kumuandaa kwa kazi kubwa zaidi.
 
“Msiwe na hofu kwangu ninyi wote ni watumishi wa Mungu, Naomba ushirikiano wenu, umoja wen una wala Dkt Samia hajaniteua kuja kuhangaika na mambo ya Makonda  ameniteua kuhangaika na itikadi uenezi wa CCM,”amesema Makonda.
 
Amesema Kamati Kuu haijakaa kwenye kikao kumtafuta mtu wa kulipa kisasi bali kumtafuta mtu wa kujenga nguvu na kujenga Imani ya Watanzania kwenye chama cha mapinduzi.
Makonda amesema CCM ni sikio na sauti ya wananchi ambapo kazi yake kubwa ni kusikiliza kwa niaba ya serikali na kusema kwa niaba ya wananchi pindi wanapokuwa na matatizo na kuyasema kwa serikali.
 
Awali Makonda amesema anatarajia kupata taarifa sahihi ili iweze kufanya kazi ya kumsaidia Katibu, Makamu, na Mwenyekiti wa Chama ili kuimarisha na kukijenga chama.
 
Akizungumza kabla ya kumkabidhi ofisi, aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema amesema anamkabidhi ofisi ili aendelee na kuhakikisha CCM inakwenda kushinda.
 
Mjema ameteuliwa kuwa Mshauri wa Rais Idara ya wanawake na makundi maalum, amesema CCM inamtegemea na kwamba ndiyo moyo ya Chama hicho.

Share To:

Post A Comment: