Na. WAF- Dar es Salam.


Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ameutaka uongozi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road kukamilisha kwa wakati ujenzi wa jengo la mradi wa PET-CT Scan na Cyclotron unaogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 18.2 ili kuleta tija ya uwekezaji uliofanywa na Serikali kwa wananchi.

Dkt. Mollel amesema hayo leo Jijini Dar Es Salaam wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya kwa wananchi na kuongea na menejimenti ya watumishi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road.

“Kamilisheni jengo hili mapema iwezekanavyo na katika ubora unahohitajika kwani Serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inahitaji uwekezaji wake kuleta matokeo chanya kwa wananchi wake”. Amesema Dkt. Mollel

Wakati akiendelea kutoa maelekezo Dkt. Mollel amesema kuwa Ujenzi wa jengo hilo ukiliangalia kwa nje unaweza kusema limegharimu kiasi kidogo sana cha fedha ila kwa ndani ndio utagundua thamani ya fedha iliyotumika kuwa inaendana na thamani ya mashine zilizosimikwa pamoja na ubora madhubuti wa jengo lenyewe.

Aidha, ameupongeza uongozi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa kusimamia vizuri fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya miradi mbalimbali ili kuboresha huduma za Afya.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dkt. Julius Mwaiselage, amemhakikishia Dkt. Mollel kumalizika mapema kwa ujenzi huo kwani kwa upande wa jengo limekamilika kwa asilimia 98.

“Mashine tayari zimekwishasimikwa kwa asilimia 100 huku tukisubiri utaratibu wa kuunganisha umeme ili mashine hizo zianze kutumika kama inavyotakiwa”. Amesema Dkt. Mwaiselage.

Vile vile amesema jengo hilo limekusanya mashine mbili kubwa ambazo ni PET-CT SCAN pamoja na CYCLOTRON (kiwanda cha kutengeneza mionzi) ambapo kwa sasa Tanzania nzima kitakuwa ni kimoja tu ambacho kitakuwa kikitengeneza mionzi ambayo itatumika kwa Taasisi huku mingine ikipelekwa kwenye hospitali nyingine kwa ajili ya kusaidia wagonjwa. 

Hata hivyo amesema kuwa kwa sasa Taasisi hiyo inanunua mionzi hiyo kutoka Afrika ya Kusini huku gharama zake zikiwa kubwa mno ukilinganisha na uwezo wa Watanzania wenyewe.

Amesema, kukamilika kwa usimikaji huo kutakuwa msaada mkubwa sana kwa Tanzania na Afrika mashariki na kati kwa ujumla.

Share To:

Post A Comment: