Shirika la Omuka Hub ambalo limeanzishwa na Mhe Mbunge Neema Lugangira kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Marekani National Democratic Institute - NDI wameandaa Majadiliano ya Jukwaa la Wanawake katika Siasa kwa lengo la kujadili Mapendekezo ya Kikosi Kazi na Maazimio ya Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama Vya Siasa yaliyotangazwa siku ya Jumatano tarehe 13 Septemba 2023.


Mjadala juu ya Ushiriki wa Wanawake katika Siasa katika ngazi zote kuanzia Kitongoji hadi Taifa umefanyika Bukoba, Mjini na umehudhuriwa na washiriki 100 kutoka makundi mbalimbali ya jamii ikiwemo Viongozi wa Dini, wakina Mama Viongozi , Wakuu wa Mashirika/NGOs, Viongozi wa Kisiasa kutoka Vyama Vya Siasa mbalimbali.

Maazimio ya Mjadala huu yanakwenda kuwa chachu katika utekelezaji wa maono ya Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Kuimarisha Uwakilishi wa Wanawake katika Siasa.

Aidha, Maazimio haya yatawasilishwa kwa Mhe Sisty Nyahoza, Msajili Msaidizi wa Vyama Vya Siasa ambae ndio Mgeni Rasmi wa Semina hii.

Washiriki wa Semina hii wamempongeza Mheshimiwa Rais kwa hotuba nzuri aliyotoa wakati anafungua Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama Vya Siasa kwani hotuba ile inaeleza uhalisia na inatoa dira jinsi ambavyo shughuli za siasa zinapaswa kufanyika nchini ili kudumisha amani, utulivu na umoja wa kitaifa.

Mhe Rais alipongezwa pia kwa Serikali anayoiongoza kwa kutekeleza sehemu kubwa ya Mapendekezo ya Kikosi Kazi na walipongeza Wajumbe wa Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama Vya Siasa kwa kufikia Maazimio yanayokuza demokrasia nchini ikiwemo kuimarisha Ushiriki wa Wanawake katika siasa, na hapa Washiriki wote wameunga mkono Mapendekezo yote ya Kikosi Kazi yaliyo katika eneo la Ushiriki wa Wanawake.

Aidha, Ndg. Sisty Nyahoza, Msajili Msaidizi wa Vyama Vya Siasa ambae ndio Mgeni Rasmi wa Semina amempongeza sana Mbunge Lugangira kwa ubunifu wake mkubwa wa kuandaa Majadiliano ya Jukwaa la Wanawake katika Siasa kwa lengo la kujadili Utekelezaji wa Mapendekezo ya Kikosi Kazi na Maazimio ya Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama Vya Siasa (trh 11-13/ Sept. 2023) katika ngazi ya jamii.

Ndg. Nyahoza amewapongeza sana washiriki kwa mjadala mzuri sana na amechukua maoni yao ambayo yatafanyiwa kazi. Kikubwa zaidi amefurahia jinsi ambavyo amekutana washiriki kutoka ngazi ya jamii wa makundi mbalimbali wana uelewa mkubwa na masuala ya Ushiriki wa Wanawake katika Siasa.

Hii imempelekea kuwaomba Shirika la National Democratic Institute - NDI kuwa Majadiliano haya ya Jukwaa la Wanawake katika Siasa aliyoanzisha Mhe Mbunge Neema Lugangira ifanyike katika ngazi ya Kata na pia Wilaya zingine, na Mikoa mingine
Share To:

Post A Comment: