Na Immanuel Msumba ; Monduli

Zaidi ya Wananchi 4,752 wa Kijiji cha Meserani  Bwawani katika Kata ya Meserani Wilayani Monduli  Mkoani Arusha waliokuwa wakilazimika kutembea zaidi ya kilomita 17 kufuata maji ya kwenye mabwawa yaliyotwama baada ya kukauka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi yaliyosababisha ukame wameondokana na adha hiyo baada ya kukamilika kwa mradi wa maji uliogharimu Milioni 549,780,722/= fedha ambazo zimetolewa na Serikali Kuu.

Maji ni muhimu kwa viumbe vyote duniani, bila maji hakuna uhai. Aidha maji ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kiwango cha maendeleo ya jamii yoyote kinategemea kuwepo kwa maji ya kutosha na yenye ubora unaotakiwa. 

Katika hali yake ya asili, maji ni sehemu ya mazingira ambapo wingi na ubora wake ndio unaosaidia katika kuamua jinsi maji yatakavyotumika. Upatikanaji wa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na usafi wa mazingira ni muhimu katika kulinda afya za wananchi. Utumiaji wa maji ambayo sio salama na uhaba wa maji huchangia katika kusababisha milipuko na kuenea kwa magonjwa kama kuhara na kipindupindu.

Katika kusaidia jamii hususani za kimaasai zilizopo vijijini katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ili kuweza kuwasaidia kupata maji safi na salama ili kuondokana matumizi ya maji yaliyotwama wananchi wa vijiji hivi ambao wengi wao wanajishughulisha na kilimo na ufugaji Serikali imeendelea na kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kuwafikishia wananchi hawa huduma ya maji.

Mradi huu ambao unasimamiwa na Wakala wa Maji Safi na usafi wa Mazingira vijijini RUWASA umehusisha tenki kubwa lenye ujazo wa maji lita laki moja na elfu thelathini na tano ambao utahudumia zaidi ya wananchi 4752 na mifugo zaidi ya Elfu 23

Mhandisi Neville Msaki ni meneja wa RUWASA wilaya ya Monduli anaeleza kuwa mradi huu ulianza kusanifiwa mwaka 2014 na wataalamu wa maji Bonde la Pangani kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa Arusha ambapo baadae mwaka 2019 ukafanyiwa mapitio na timu ya usanifu ya RUWASA mkoa.

“Mwaka jana tulianza ujenzi wa mradi huu ambapo tumefanikiwa kulaza bomba kilomita 17.8 na kujenga vituo 8 vya wananchi kuchota maji na piatuliweza kujenga malambo moja ya kunyweshea mifugo maji ili kuwaondolea wananchi adhan a kuwatua ndoo kichwani” Alisema Msaki

“Tunamshukuru sana Rais Samia kwa kuendelea kuwajali wananchi wa Monduli wanaokabiliwa na ukame kwa kuendelea kutupatia fedha za utekelezaji wa Miradi yam aji Wilayani hapa ili kuhakikisha anaendelea kumtoa mama ndoo kichwani” Aliongezea 

Mradi huu unahudumia wananchi zaidi 4752 wa Kijiji cha Meserani Bwawani, Zahanati, Shule ya Sekondari, Shule ya Msingi na Vijiji vya jirani vya Engorika, Lengiloriti na Moita Kipok.

Lekisarisho Oitesoi ni Mkazi wa Kijiji cha Engorika ambapo anaeleza kuwa kwa hiki kinachofanyika sasa tuna kila sababu ya kumpongeza Rais wetu, Samia Suluhu Hassan tumepata maji safi na salama kwa ajili ya afya zetu lakini tunampongeza waziri wetu wa maji kwa kuweka msukumo mkubwa kwenye miradi hii ya maji inayotekelezwa katika wilaya yetu hakika sasa mifugo itaenda kupata maji.

"Shida ya maji ilikuwa ni kubwa, tunashukuru serikali kutuletea  huu mradi maana mwaka jana kipindi kile cha ukame  tulikuwa hatuna maji kabisa serikali ilikuwa inatuletea na magari kupitia kwa mwenyekiti wa Kijiji lakini yalikuwa hayakidhi mahitaji yetu maana kwenye maboma yetu tupo wengi sana,yaani tulikotoka kulikuwa ni kugumu kulikuwa na  hali mbaya tunashukuru sana kwa kweli” Alisema Oitesoi.

"Niwapongeza sana ndugu zangu RUWASA kwa kazi kubwa na zuri unayoifanya ya kuhakikisha sisi wananchi tunaoishi vijiji tunapata maji safi na salama"

Sara Oltetia ni mama wa watoto watatu ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Bwawani ambapo anaeleza kuwa alikuwa anatumia muda wake mwingi akiwa amebeba Watoto mgongoni huku akiswaga punda kutembea umbali mrefu kufuata maji yaliyotwama kwenye mabwawa ila kwa sasa anasema ananufaika vyema na mradi wa maji unaowahudumia kijijini hapo.

"Ninampongeza mama Samia Suluhu Hassan ametutua ndoo kichwani, ameisaidia jamii yetu ya kifugaji Meserani kulikuwa na changamoto kubwa sana ya maji, lakini tunashukuru tangu kukamilika kwa lile tenki na kujengewa sehemu za kuchota maji  mpaka sasa tuna maji safi na salama kwa muda wote yanatoka." Alisema

“Uwepo wa huduma hii utatusaidia sisi wananchi wa Kijiji hichi na vijiji vya jirani adha  dhidi ya kupata magonjwa ya mlipuko na tumbo kutokana na uwepo wa maji Safi kwenye makazi yetu kwa sasa maana hapo awali tulikuwa tunatumia maji ya kwenye mabwawa na mifugo” Alisema

Naye diwani wa kata ya Meserani Loth  Tarakwa ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo katika kata yake hususani mradi huu mkubwa wa maji ambao umekwenda kusaidia wananchi wa Kata hiyo na vijiji vya Jirani.

“Kukamilika kwa mradi wa maji wa Kijiji cha Meserani Bwawani kutawasaidia wananchi wangu Kwenda kujihusisha na masuala ya mbalimbali ya maendeleo zaidi badala ya kwenda kutafuta maji kwani hapo awali walikuwa wanatumia muda mwingi Kwenda kutafuta maji kwa kutembea umbali mrefu zaidi ya kilomita 17” Alisema Diwani

“Kwa sasa RUWASA waendelee kutusaidia kufikisha haya maji katika maeneo mbalimbali ya Viijiji vyetu sambamba na kutujengea malambo kwa ajili ya kunyweshea mifugo yetu wakati wote wa kiangazi na masika” Aliongezea

Pia mnafahamu Wilaya yetu ya Monduli inakabiliwa sana na mabadiliko ya tabia nchi tunaendelea kuiomba Serikali kuendelea kufikisha maji katika zile kata ambazo nazo zinakabiliwa sana na ukame ambapo mifugo na wananchi wanapata shida wanaacha kufanya shughuli za kujiingizia kipato na kutumia muda mwingi kwenda kusaka maji.

Share To:

Post A Comment: