Na John Walter-Arusha

Baadhi ya Wananchi waliosalia ndani ya mamlaka ya Hifadhi ya  Ngorongoro (NCAA) wamewaambia Waandishi wa Habari kuwa wanaishi katika maisha ya tabu yasiyokuwa na huduma za kijamii na kwamba wanatamani kuondoka.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika kata za Nainokanoka na Naiyobi, wameeleza kuwa wanataka kuondoka kwa hiari kuwafuata wenzao katika makazi mapya ya Msomera huku wakiiomba serikali ya rais Samia ifanye hivyo haraka kwa kuwa hawaoni sababu ya kuendelea kuishi katika maeneo hayo.

"Baada ya kuona mazingira na maisha wanayoishi wenzetu tumehamasika na sisi tunaomba tuondoke,tupo tayari hata leo" alisema Kesuma Torume 

Sinyati Emmanuel na Marry Kesumo Wanasema hawawezi kuishi mahali ambapo hakuna bara bara nzuri, maji,hospitali wala usafiri na kwamba hawana shughuli za maendeleo wanazozifanya kwa kuwa hawaruhusiwi hata kulima katika maeneo hayo.

"Tukitoka kuokota kuni hatuna kazi nyingine ya kufanya, tunakaa tu kusubiri mifugo itoke machungani,hakuna kitu tunafanya" alisema Marry

Naye Jennifer Yuda kutoka kijiji cha Kapenjiro kata ya Naiyobi ambaye yupo tayari kuhama kwa hiari kutoka Ngorongoro kwenda Msomera, ameiomba serikali iwapatie maeneo kutokana na idadi ya Wake waliopo katika Boma husika.

 Mosses Lenara ameishukuru Serikali kwa upendeleo ilioutoa kwao kwa kuwajengea nyumba Msomera na kuwapatia maeneo ya kilimo na ufugaji.

"Mimi na Boma yangu yote tupo tayari kuhama,  huku jamani ni  porini hakuna maendeleo tunafanya" alisema Lenara

Serikali ilitoa nafasi ya kuwahudumia kila kitu ikiwa ni pamoja na kuwajengea Nyumba, Shamba na maeneo ya malisho, kuwasafirisha wao, mifugo na mizigo yao wote waliokubali kuhamia Msomera mkoani Tanga kwa hiari ili kupisha eneo hilo ambalo ni makazi ya wanyamapori wanaoingizia nchi mapato kupitia watalii.


Share To:

Post A Comment: