Na; Elizabeth Paulo, Dodoma 

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) inatarajia kuwakutanisha wahitimu wa Programu ya Kukuza Ajira na Ujuzi kwa Maendeleo Afrika (E4D) na waajiri ili kushirikishana katika fursa za soko la ajira kwa kuandaa kongamano litakalofanyika jijini Dodoma.


Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Abdallah Ngodu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano hilo linaloandaliwa kwa kushirikiana na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (GIZ) litakalofanyika Agosti 24 jijini Dodoma.


Bw. Ngodu amesema kuwa kupitia Kongamano hilo wanafunzi/wanufaika watakutanishwa na waajiri ili waweze kushirikishana kuhusu taarifa za soko la ajira. Halikadhalika Wahitimu wataonesha umahiri wa ujuzi wao katika bidhaa walizotengeneza na miradi yao wanayotekeleza,”


Na kuongeza kuwa “kupitia kongamano hili wananchi watapata fursa ya kujionea shughuli zinazofanywa na wahitimu/wanufaika wa mradi wa E4DT pamoja na kupata taarifa juu ya fursa za mafunzo ya ufundi stadi zinazopatikana kwenye vyuo vya VETA nchini,”ameeleza Bw.Ngodu Aidha amesema hadi sasa jumla ya vijana 3,258 wamenufaika na mafunzo katika vyuo vya VETA vya Dodoma, Manyara, Lindi, Singida, Mikumi, Gorowa na Dakawa katika awamu nne (4) huku udahili wa awamu ya tano ukiendelea na mafunzo hayo yametolewa kwa wiki nane (8) vyuoni na wiki nane (8) mahali pa kazi.


“Inatarajiwa nguvukazi yenye ujuzi kutokana na mradi wa E4D itatumika katika kukuza ajira kwenye miradi ya kimkakati ya uwekezaji kama vile bomba la mafuta, bwawa la Nyerere na Treni ya mwendokasi.Mradi huu unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2023,”amesema Bw.Ngodu 


Wakati wa kongamano hilo kutakuwa na maonesho ambayo yamelenga kujenga uelewa juu ya fursa za ufundi stadi zilizopo kwenye Mradi, kukuza uwezo wa kuajirika (Kujiajiri/Kuajirika) kwa wahitimu/wanufaika wa kozi zinazotolewa na Vyuo vya VETA chini ya Mradi wa E4DT.Amesema kwenye kongamno hilo pia kutakuwa na taasisi za fedha ambazo zitatoa fursa za uwezeshwaji hususani mikopo inayoweza kuwanufaisha vijana waliopata ujuzi ili wawe na mitaji ya kuendesha shughuli za uzalishaji na kuongeza vipato na ajira endelevu.


Tanzania ni miongoni mwa nchi sita za Afrika zinazotekeleza mradi wa Stadi za Ajira kwa Maendeleo Afrika (E4D) unaofadhiliwa na Wizara ya Shirikisho la Ujerumani la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (BMZ) na Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la Korea (KOICA). Mradi wa E4DT ulianza kutekelezwa mwezi Mei, 2022, ukilenga kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa vijana 4000 nchini, katika fani za Ufundi Bomba wa majumbani (Domestic Plumbing), Ufundi Bomba Viwandani (Industrial Plumbing), Ufundi wa Uchomeleaji Vyuma Viwandani (Industrial Welding) na Ufundi wa Mekatroniki (Mechatronic). 


Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo Cha ufundi Cha Veta Dodoma Stanslaus Ntibara ,amesema hadi kufikia tarehe 19 mwezi huu jumla ya wanafunzi 1806 wa Mkoa wa Dodoma waliokuwa wameshahitimu mafunzo hayo.Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: