Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha Sekta ya Afya kwa kuajiri watumishi wapya wa afya takribani 29,000 katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa madarakani, huku asilimia 80 wakiwa wamepelekwa kwenye Zahanati, vituo vya Afya na na Hospitali za Wilaya.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe kwa niaba ya Waziri wa Afya wakati wa Kikao cha 73 cha Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Africa (WHO Afro) kilichoanza tarehe 27 Agosti 2023 jijini Gaborone Botswana ambacho kimewakutanisha Mawaziri wa Afya, watendaji na viongozi wa mashirika ya afya Katika nchi za Kiafrika.

Akiongea kwa niaba ya Waziri wa Afya na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Grace Magembe, aliwaambia wajumbe kuwa Tanzania chini ya uongozi wa  Mheshiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imepiga hatua katika uimarishaji wa huduma za Afya ya msingi baada ya uwekezaji mkubwa katika miundombinu, vifaa tiba, ununuzi wa dawa na ajira ya  watumishi takribani elfu 29 ndani ya miaka miwili. 

"Kutokana na uboreshaji wa upatikanaji wa huduma za afya Tanzania, Hadi kufikia mwaka 2022 asilimia 70 ya watanzania wanapata huduma za afya ndani ya kilometa tano kutoka kwenye maeneo wanayoishi”. Amesema Dr Magembe.

Aidha, Dkt. Magembe amewaambia wajumbe wa kikao kuwa Tanzania kwa sasa inaandaa mpango na Taasisi ya Susan Thompson Buffet Foundation (STBF) wa kuimarisha huduma za watoa huduma za Afya  ngazi ya jamii ili waweze kutoa huduma zote kwa pamoja ikiwemo za afya ya uzazi na mtoto, afya ya uzazi kwa vijana, chanjo, lishe, usafi wa mazingira, rufaa, magonjwa yasiyo ya kuambukiza na ya kuambukiza. 

Ameongeza kuwa watoa huduma hao watapatiwa mafunzo kwa muda wa miezi 6 na idadi yao inatarajiwa kuwa zaidi ya laki moja na nusu ambao watapatikana kutoka kwenye vijiji na mitaa yao wanayoishi kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI na mamlaka za uongozi wa maeneo husika.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa STBF, Bwana Tewodros amesema Taasisi yake ipo kwenye hatua za mwisho za kupitia andiko la WAJA la Tanzania na hivi karibuni wataleta mrejesho wa namna mradi huo utakavyotekelezwa kati yao na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Share To:

Post A Comment: