Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja amezindua hoteli ya Home Ground katika Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi itakayosaidia kukuza Mtandao wa Utalii katika eneo la huduma na malazi  kwa watalii wanaokuja nchini.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhe. Masanja amesema kuwa uwekezaji  wa hoteli  hiyo unaenda kusaidia Hifadhi ya Taifa Katavi ambayo ni moja kati ya  hifadhi ya tano kwa ukubwa nchini ikiwa yenye kilomita za mraba 4,471. 

Ameongeza kuwa uzinduzi wa hoteli hiyo ni mwendelezo wa ushirikiano baina ya Serikali  na  Sekta Binafsi katika utoaji wa huduma za malazi nchini.

“Tukio hili linaonesha dhahiri umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kutoa huduma za kitalii na pia linaunga mkono juhudi thabiti za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan  kama alivyoeleza katika uzinduzi wa filamu ya  "The Royal Tour " “tunapenda kuwakaribisha wawekezaji wengine kwani Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutangaza utalii duniani na kufungua milango kwa nchi nyingi kutembelea Tanzania ” Mhe. Masanja amesema.

Aidha, ametumia fursa hiyo kutoa  pongezi  kwa uwekezaji huo mkubwa uliofanyika, huku  akisema  idadi na viwango vya huduma za malazi imeongezeka.

"Sisi kama  Serikali tutazidi kuweka mazingira wezeshi  ili kudumisha ushirikiano mkubwa katika kukuza na kuongeza idadi wa watalii wanaofika katika hifadhi hii ya Katavi, wekezeni kwenye huduma za malazi " amesisitiza Mhe.Masanja.

Naye Mwenyekiti wa Bodi wa Hoteli ya Home Ground,  Mhe. William  Mbogo amesema ujenzi wa Hoteli hiyo uliogharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.5 ulianza mwaka 2019 na unatarajiwa kutumia takribani bilioni 4 mpaka kukamilika kwake.

Amesema uwekezaji huo utasaidia kuchangia katika mapato ya Serikali kwa kodi mbalimbali inayolipa lakini pia umetoa ajira kwa vijana takribani 40 wa Kitanzania. 

Mbogo ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuboresha miundombinu ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi pamoja na kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza ndani ya hifadhi hiyo.

Share To:

Post A Comment: