Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja ameitaka Menejimenti ya  Hifadhi ya Taifa Katavi kuainisha maeneo ya uwekezaji huku akisisitiza utangazaji wa kimkakati katika maeneo hayo ufanyike  ili kuwavutia Wawekezaji wa ndani na nje nchi kuwekeza katika Hifadhi hiyo 

 Ametoa kauli hiyo leo wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Makao Makuu ya Hifadhi hiyo, ambapo amesema utangazaji wa maeneo hayo utawavutia Wawekezaji kuwekeza katika ujenzi wa  huduma za malazi ya watalii. 

"Ainisheni maeneo hayo kwani  Wawekezaji wengi wanataka kuwekeza katika Hifadhi hii " Mhe. Masanja amesisitiza.

Akizungumzia faida ya kutangaza maeneo watakayoainisha, Mhe.Masanja amesema  miundombinu itaboreka pamoja na  mazingira yatawavutia watalii wengi kuja  kutembelea na kulala hifadhini humo 

Katika hatua nyingine, Mhe.Masanja ameendelea kuwasisitiza Wananchi kuacha kuvamia maeneo ya Hifadhi huku akiwataka  wahifadhi kuendelea  kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa maeneo hayo kitaifa na kimataifa.

"Ili kuendelea kuwa na mahusiano mazuri na Wananchi wetu,  Nawaomba nendeni mkatoe elimu kwa wananchi wasisogelee maeneo ya hifadhi na hapo walipo wasiendelee kuongeza maeneo" Mhe. Masanja amesema

Hifadhi ya Taifa Katavi ni hifadhi ya tano kwa ukubwa kati ya hifadhi 21 nchini ikiwa na kilomita za mraba 4,471.

Share To:

Post A Comment: