NA DENIS CHAMBI, TANGA.

JESHI la Polisi mkoa wa Tanga limefanikiwa kuwakamata watu kumi na moja  wakiwemo wanawake wawili na wanaume tisa  wakazi wa Dar es salaam waliokuwa wakijihusisha na wizi wa fedha kwa njia ya simu ambapo wamekuwa wakituma ujumbe  kwa watu mbalimbali wakiwataka wawatumie fedha  bila ridhaa yao.

Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari kamanda wa jeshi la Polisi mkoa wa Tanga Henry Mwaibambe amesema kuwa watuhumiwa wote walikuwa wakiishi katika nyumba moja waliyokuwa wamepanga maeneo ya Donge Kata ya Mnyanjani jijini hapa ambapo wote wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili. 

Kamanda Mwaibambe aliongeza kuwa watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na vitu mbalimbali ikiwemo  laini za simu 42 vocha mbili zenye thamani ya shilingi 2,000 karatasi  43 zilizoandikwa namba za simu na namba za mawakala wa mitandao ya fedha,  kadi tano za benki mbalimbali, vitambulisho 14, na betri za simu ndogo 7.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni  Hadija Nyange (34) mkazi wa Muheza, Zaina  Athuman (25) mkazi wa Mwazange, Innocent Omeme (35),Abdulazizi Nzori (31),Said Hassan (24), Rashid Habibu (23), Said Juma (30), Idd Kaniki (35), David Rupiana (22), Salum Salum (24) wote wa kutoka Dar es salaam pamoja na Omary Mohammed (27) mkazi wa Mkanyageni Tanga ambapo wote wamefikishwa mahakamani.

"Jeshi la Polisi mkoa wa Tanga limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 11 ambao wanajihusisha na uhalifu kwa njia ya mtandao ambao hutuma ujumbe mfupi wa maneno kwa watu mbalimbali wakiwataka watume pesa, baada ya kukamatwa walikutwa na fedha tathlimu milion mbili na elfu themanini na tani  (2,085,000), pesa ya Congo elfu arobaini na tano na mia moja  (450,100) , simu kubwa 11, simu ndogo 13 kadi 5 za benki mbalimbali, " alisema

"Aidha  katika ufwatiliaji  jumla ya laini za simu 441 walizokuwa nazo watuhumiwa kwa lengo la kuwatapeli watu mbalimbali kwa kuziorodhesha namba za simu na majina ya watumiaji, laini 399 za simu baada ya kufanya utapeli walizichoma moto na kati ya laini hizo 183 zilitumiwa ujumbe mfupi wa maneno na kumtaka mwananchi atume pesa , laini 42 za simu zilikuwa katika mchakato wa kuwatapeli watu mbalimbali watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani kujibu mastaka yanayowakabili" alisema Kamanda Mwaibambe.

Hata hivyo Kamanda Mwaibambe amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la Polisi ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu pale wanapowaona katika maeneo yao ili kuendelea kudumisha amani na usalama nyakati zote.

"Hawa watu ni watu hatari sana tusiposhirikiana na jeshi la Polisi hatuwezi kuwafunga wakitoka hapa wanaweza kwenda kutapeli na kwingineko, tunaomba sana mtoe ushirikiano katika kukomesha  vitendo hivi" aliongeza.

Katika hatua nyingine kwenye barabara ya Same maeneo ya Chekelei mkoani Tanga  jeshi hilo limefanikiwa kukamata watu watatu wakiwa  na gari waliokuwa wamebeba  bunda 313 za madawa ya kulevya aina ya Milungi  zenye uzito wa kilo 112.05.

"Jeshi la Polisi mkoa wa Tanga tunaendelea na juhudi za kupambana na madawa ya kulevya  , tumefanikiwa  ndani ya mwezi huu wa 7 barabara ya Tanga kwenda Same  maeneo ya Chekelei tuliweza kukamata watuhumiwa watatu wakiwa kwenye gari zenye usajili namba T 417 CJS walikutwa wakiwa ndani na madawa ya kulevya  aina ya Milungi bunda 313 zenye uzito wa kilo 112.05  tayari taratibu za kisheria zishafanyika  kielelezo tumepeleka kwa mkemia mkuu wa serikali amethibitisha kuwa ni madawa ya kulevya aina ya Milungi" alisema Kamanda




 

Share To:

Post A Comment: