Na. Damian Kunambi, Njombe.

Mkuu wa wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva amezindua Zahanati ya kijiji cha mkiu kilichopo wilayani humo Mkoani Njombe ambapo ujenzi wake umechangiwa na nguvu ya wananchi kiasi cha Sh. Mil. 22.5 huku serikali kuu ikitoa sh. Ml. 50.

Akisoma taarifa ya ujenzi wa zahanati hiyo afisa mtendaji wa kijiji hicho Daniel Henjewele amesema sanjari na michango hiyo ya wananchi na fedha kutoka serikali kuu lakini pia Halmashauri ya wilaya hiyo pia ilitoa fedha kiasi cha zaidi ya sh. Mil. 29 ambazo zimetumika katika kukamilisha miundombinu ya majengo, ununuzi wa vifaa tiba na kusaliwa na kiasi cha sh. Mil. 10.4.

Aidha kwa upande wake mganga mkuu wa wilaya ya Ludewa Stanley Mlay amesema kwa sasa zahanati hiyo itaanza kutolewa huduma ikiwa na wahudumu wawili wakati wakiendelea kufanya mchakato wa kuongeza wengine hivyo amewaomba wanachi kuwapa ushirikiano wahudumu hao kwani wataenda kuwapa hudumba mbalimbali za kiafya. 

" Huduma zitakazotolewa hapa ni huduma za uzazi, matibabu ya wagonjwa wa nje, huduma za chanjo, upimaji virusi vya ukimwi pamoja na matibabu pamoja huduma za ngazi ya jamii ambazo hutolewa kwaajili ya wagonjwa ambao hawana uwezo wa kufika katika zahanati".

Hata hivyo kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva amewataka wahudumu hao wa afya pamoja na uchache wao kutoa huduma nzuri na zinazostahili na kutokutoa kauli zenye kuudhi kwa wagonjwa wanaofika katika zahanati hiyo.

"Najua kwa sasa mmeletwa wahudumu wawili tu kuanza kutoa huduma hapa, kwa idadi yenu najua muda mwingine mnaweza kuzidiwa na wingi wa wagonjwa ambao wote wanategemea huduma yenu, sasa niwaombe mkawe na kauli nzuri kwa wagonjwa na kuwapa huduma stahiki wakati serikali ikiendelea kuona uwezekano wa kuleta wahudumu wengine zaidi".

Pia aliwapongeza wananchi kwa kujitolea kuanzisha ujenzi wa zahanati hiyo na kusema kuwa serikali inatambua mchango wao na ndiomaana imewaunga mkono katika ukamilishwaji wa zahana hiyo.

Vilevile kwa upande wa wananchi wa kijiji hicho wameishukuru serikali kwa kuwakamilishia zahanati hiyo kwani itaenda kuwapunguzia umbali mrefu waliokuwa wakitembea awali katika kufuata huduma ya afya.

Share To:

Post A Comment: