Afisa Vijana Mkoa wa Singida  Frederick Ndahani (wa pili kushoto) akiwa na wajumbe wa Kamati ya Lishe wa Shule ya Msingi Nkalankala na Shule ya Sekondari ya Set Benjamin wakati akikagua chakula kilichopatikana kwa ajili ya wanafunzi wa shule hizo. 

Na Mwandishi Wetu, Singida 

AFISA Vijana Mkoa wa Singida  Frederick Ndahani ameupongeza Uongozi wa Shule ya Msingi Nkalankala na Shule ya Sekondari ya Set Benjamin pamoja na wazazi  wa Kata ya Nkalankala kwa kuamua kutoa chakula kwa wanafunzi shuleni.

Ndahani ameyasema hayo wakati akifuatilia Ufundishaji na hali ya utoaji wa chakula shuleni katika Shule za Msingi na Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida.

Ndahani amewapongeza wazazi waliounda kamati ya Lishe ya shule na kusimamia ,utoaji wa elimu ya umuhumu wa chakula,ukusanyaji,utunzaji na upishi ambapo hadi sasa Shule ya Msingi Nkalankala imekusanya jumla ya magunia 90 ya Mahindi, maharage gunia 20 na mafuta ya chakula lita 350 na Shule ya Sekondari Set Benjamin tayari imekusanya magunia 33 ya mahindi,maharage gunia 12 ,mafuta ya chakula lita 150 na sukari kilogramu 25 hatua ambayo imesaidia wanafunzi wote katika shule hizo kupata chakula shuleni.

Nawashauri viongozi na wazazi kuiga mfano wa wazazi wa Nkalankala katika utoaji wa chakula shuleni na tukiamua tunaweza kuleta mapinduzi ya elimu mkoani Singida kwa sababu watoto sasa watapata chakula na kuwa watulivu darasani.

Kwa upende wake Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe katika Shule ya Sekondari Set Benjamin Abduli Silimu amesema wazazi baada ya kushirikishwa jambo hilo la uchangiaji wa chakula wamekubali  kutoa chakula cha kutosha ambacho kitatumika hadi msimu ujao wa chakula wa Juni 2024.

Katibu wa Kamati ya Lishe katika Shule ya Msingi Nkalankala,  Elizabeth Yona amesema wajibu wa wazazi ni kutoa huduma bora kwa watoto.

" Serikali ina wajibu wake, walimu na Sisi wazazi tunaowajibu wetu na moja ya wajibu ni kuwapatia chakula wanafunzi wakiwa shuleni na nje ya shule," alisema Yona.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Set Benjamin Jackiline Molel na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nkalankala iliyopo Mkalama wamesema wataendelea kusimamia utoaji wa Chakula Shuleni Kwa kushirikiana na Wazazi wa Kata ya Nkalankala.

Afisa Vijana Mkoa wa Singida  Frederick Ndahani (katikati) akiwa na wajumbe wa kamati hiyo ya Lishe ya shule hizo wakikagua chakula hicho.
 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: