NA DENIS CHAMBI, TANGA.

 MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyama pori Tanzania 'TAWA' imewaomba waandaaji na  maonyesho ya biashara na utalii Tanga ambao ni chemba ya biashara 'TCIAA' kuendelea kuboresha mazingira yatakayosaidia na  kuwavutia wafanyabiashara, wawekezaji, taasisi , makumpuni , wajasiriamali mbalimbali na wananchi kwa ujumla na hatimaye  kuweza kushiriki kwa wingi maonyesho hayo ambayo hufanyika kila mwaka katika viwanja Mwahako.

Ombi hilo limetolewa na afisa mhifadhi mwandamizi kutoka mamlaka ya Usimamizi wa  Wanyama pori Tanzania 'TAWA' Proches Rongoma mara baada ya kufungwa rasmi kwa maonyesho ya 10 biashara na utalii yaliyofanyika kwa siku 10 katika viwanja vya Mwahako jijini Tanga na mkuu wa mkoa huo Waziri Kindamba June 6, 2023.

Rongoma  alisema kuwa idadi ya  watalii na wananchi waliojitokeza kuangalia wanamnayama mbalimbali katika bustani iliyopo kwenye viwanja hivyo haikuwa  kubwa kama ilivyotarajiwa hii ni kutokana na hali ya  hewa ambapo mvua zilinyesha kwa wingi hivyo kupelekea washiriki wengi kushindwa kufika katika maonyesho hayo.

"Tuliwaambia waandaaji wa maonyesho ya biashara na utalii ambayo ni chemba ya biashara Tanga kutengeneza mradi wa kudumu ambao utaonekana kama maeneo mengine ya maonyesho, kutengeneza mazingira yote ya maonyesho kila banda ili kuweza kuwavutia watalii  na wafanyabiashara wengi zaidi kwa maonyesho yajayo" 

"Maeneo ya mabanda yajengwe katika namna ambayo yatapauliwa na mabati ili yasiharibike mapema yawe ya kudumu tunategemea kwamba  wataweza kuboresha eneo hili hasa kunapokuwa na mvua nyakati zote  kwa sababu ukiangalia kwa mwaka huu mvua zimeathiri sana tumekosa watalii wengi zaidi ya vile ambavyo tulitegemea" alisema Rongoma.

Akizungumzia maonyesho hayo ya biashara na utalii ya 10 kufanyika jijini Tanga Afisa huyo alisema kuwa kila mwaka TAWA wamekuwa wakiyaboresha kwa kuongeza wanyama pori na ndege wa aina tofauti tofauti hii ikilenga zaidi kuwavutia watalii wa ndani na hatimaye kutembelea  hifadhi mbalimbali zilizopo hapa nchini.

"Maonyesho ya mwaka 2023 yamekwenda kwa namna ya tofauti zaidi kwa upande wetu TAWA tuliyaboresha kwa kuwaletea Wanyama pori na ndege wa tofauti tofauti na wananchi waliotembelea maeneo haya na kuwaona wanyama na ndege na wamefurahia kuwaona na hiyo yote ni kwaajili ya kuzitangaza hifadhi za Tanzania" aliongeza.

Kwa upande wake  Afisa mhifadhi  daraja la pili kutoka Mamlaka ya usimamizi wa wanyama pori Tanzania TAWA  Veronica Mollel amesema ushiriki wao wa kila mwaka katika maonyesho hayo umekuwa na mchango mkubwa katika kuzitangaza hifadhi za Tanzania ambapo wananchi wengi na wadau wamehamasika na kuweza kuzitembelea mbuga mbalimbali zilizopo.

"Ushiriki wetu katika maonyesho haya ya biashara na utalii yanayofanyika kila mwaka hapa jijini Tanga umekuwa na tija sana kwa jamii wananchi wengi wamekuwa wakihamasika  ukiangalia asilimia kubwa waliokuwa wanakuja katika maonyesho haya waliokuwa wanakuja kuona wanyama kwahiyo  sisi Kama TAWA kuwepo hapa  tumehamasisha watalii wengi zaidi kuzitembelea hifadhi na mbunga mbalimbali zilizopo"

Aliongeza kuwa kila mwananchi au taasisi inaturusiwa kujenga  vitalu na bustani za kufugia wanyama wa aina tofauti tofauti isipokuwa kwa kufuata sheria ambazo ni pamoja na kuwa na leseni ya biashara eneo lenye vigezo vinavyokidhi. 

Yasin Mndeme ambaye ni mmoja wa wananchi waliojitokeza katika maonyesho hayo pamoja na kufanya utalii wa ndani katika bustani ya wanyama pori na ndege  alisema ni  kuwaona  fahari kwao kuwaona wanyama ambao ni adimu  hivyo  kuiomba serikali pamoja na waandaaji wa maonyesho hayo  kuangalia namna ya kuweza kuongeza siku ikiwezekana  kufanyika mara mbili kwa mwaka.
 
Afisa mhifadhi mwandamizi kutoka mamlaka ya Usimamizi wa  Wanyama pori Tanzania 'TAWA' Proches Rongoma akitoa maelezo kwa  mkuu wa mkoa wa Tanga Waziri Kindamba (wa kwanza kulia ) kuhusu utendaji wa mamlaka hiyo wakati wa kufunga maonyesho ya 10 ya biashara na utalii yaliyofanyia katika viwanja vya Mwahako, wa kwanza kulia ni mwenyekiti wa chemba ya biashara (TCIAA) mkoa wa Tanga Rashid Mwanyoka.

Baadhi ya wanachi na wakazi wa jiji la Tanga wakiangalia wanyama waliopo kwenye vitalu vilivyowekwa na mamlaka ya usimamizi wa wanyama pori TAWA kwenye maonyesho ya biashara na utalii.

Afisa mhifadhi daraja la pili kutoka Mamlaka ya usimamizi wa wanyama pori Tanzania 'TAWA'  Veronica Mollel akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ushiriki wao kwenye maonyesho ya 10  ya biashara na utalii yanayofanyika kila mwaka katika viwanja vya Mwahako jijini Tanga.

Share To:

Post A Comment: