Na Gift Mongi : DODOMA

Katika kuhakikisha wananchi wa jimbo la Moshi Vijijini wanapata huduma stahiki na kwa wakati mbunge wa jimbo hilo Prof Patrick Ndakidemi ameendelea kuitaka serikali kuhakikisha kunakuwepo na uhakika wa mawasiliano ya barabara.

Mbunge huyo kwa mara kadhaa amekuwa akiitaka serikali kuzijenga barabara katika jimbo hilo kwa kiwango cha lami lengo likiwa ni kurahisisha shughuli za usafirishaji na mawasiliano kwa ujumla.

Mbunge huyo amehoji Bungeni je Serikali ina mkakati gani kukamilisha barabara ya Kibosho Shine hadi kwa Rafaeli kwa kiwango cha lami.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya alisema kuwa, barabara hiyo inahudumiwa na wakala wa barabara nchini Tanroad lakini kipo kipande kinahudumiwa na wakala wa barabara vijijini Tarura.

Mhandisi Kasekenya alisema kuwa, kwa upande wa Wakala wa barabara Tanroad ni mpango wao kuhakikisha wanaijenga yote kwa kiwango cha lami na hadi sasa mkandarasi yupo eneo la mradi.

Alisema kuwa, wizara katika mwaka wa fedha 2023/2024 wametenga fedha kuendelea na ujenzi kwa awamu kwa kiwango cha lami ili kukamilisha barabara yote.

Hatua hiyo imepokelewa kwa shangwe kubwa na wananchi wa kata za Kibosho ambao wanaitegemea barabara hiyo kuwaletea maendeleo yao.

Godlisten Mallya mkazi wa Kibosho Mande alisema kupatikana kwa barabara zenye  uhakika ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi katika eneo lao.

'Tukipata barabara ambazo zinaweza kutumika kipindi chote ni kichocheo kimojawapo katika kukuza uchumi lakini pia maendeleo yatakuja Kwa Kasi tofauti na sasa'alisema

Share To:

Post A Comment: