Na Elizabeth Paulo, Dodoma 


Mbunge wa Jimbo la Mvumi Jijini Dodoma na Mjumbe wa Halmashauri kuu Ya Chama Cha Mapinduzi -NEC, Livingstone Lusinde amekemea vikali kauli zinazotolewa na baadhi ya watu au wanasiasa wanaojaribu kupotosha taarifa za uwekezaji katika bandari ya Dar es salaam.


Lusinde amesema hayo leo jijini Dodoma wakati wa mkutano na waandishi wa Habari huku akiwashauri wanasiasa na wachambuzi kuacha kutumia lugha za kibaguzi katika kupinga baadhi ya mambo yanayofanywa na Serikali kwani bila kuchukua tahadhari taifa linaweza kuingia katika migogoro.


Amesema kwa sasa taifa liko kwenye mjadala mkubwa kuhusu mkataba wamashirikiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu Bandari ya Dar es Salaam.


Jana Jumatano Juni 7,2023, Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia Na Maendeleo (CHADEMA) Freman Mbowe alitoa tamko akiwa nchini Italia ambapo alimwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuondoa azimio hilo bungeni kwa dharura ili kupisha mashauriano ya muafaka wa kitaifa juu jambo hilo nyeti.


Kufuatia Kauli hiyo Lusinde amemuwakia Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe kwa kauli yake kwamba Mkataba wa ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai katika uendeshaji wa bandari una viashiria vyote vya kuhatarisha usalama wa Nchi kiuchumi na kisiasa.



Lusinde amesema alichokisema Mbowe hakikubaliki kwani kinaleta ubaguzi na kwamba Mkataba huo kutokuwekwa wazi, Serikali inafanya mambo yake kwa siri na haiwezi kukiweka wazi kila kitu .



Mbowe aliwataka wawakilishi wa wananchi kutopitisha azimio hilo hadi uwepo wa uelewa kwani kupitisha kwao ni kuruhusu michakato mengi kuendelea.



Hata hivyo Spika Dkt.Tulia Akson mapema leo bungeni alisema azimio la Bunge kuhusu kuridhia ushirikiano wa uendelezaji na uboreshaji wa utendaji wa bandari Tanzania, litawasilishwa bungeni Juni 10, 2023 kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa na wabunge.


Azimio hilo ni mapendekezo ya kuridhia makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya katika uendelezaji na uboreshaji wa utendaji wa Bandari Tanzania la 2023.


Mbunge huyo amesema kuwa amewasikia ACT Wazalendo kupitia Zito Kabwe bila shaka uchambuzi wao ni wa kitaifa zaidi na wenye nia njema kuliko Mbowe,Mbowe anasema Rais anatoka Zanzibar na Waziri anatoka Zanzibar ila bandari ni ya Dar es Salaam



“Kauli hii inaweza ikaharibu Muungano kwanini Bandari ya Zanzibar haihusiki haya ni maneno ambayo sio ya kiungwana,Mbowe anataka kutuaminisha ni kosa Rais na waziri kutoka Zanzibar huu ni ubaguzi.”anahoji


Katika upande mwingine Lusinde ameipongeza serikali kwa kuwaza uwekezaji katika eneo la Bandari ya Dar es salaam, huku akitaja faida za uwekezaji huo kuwa ni pamoja na kupungua kwa urasimu wa kuchelewa kwa mizigo na kuongeza mapato ya Bandari kutoka shilingi Trilioni-7.7 hadi kufikia zaidi ya shilingi Trilioni-20 huku kukiwa na kuongezeka kwa fursa za ajira.



Aidha, amepongeza Rais Dokta Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kuridhia Bunge lijadili na kupitisha maazimio yatakayoletwa na serikali katika uwekezaji, jambo ambalo linafanyika kwa mara ya kwanza.


Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: