Wafugaji kutoka wilaya ya Monduli Mkoani Arusha wamesema Mabadiliko ya tabia ya nchi yamekuwa chanzo cha umaskini katika jamii hiyo kutokana na mifugo yao kukosa malisho na Maji.


Madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanapozidi kuwa mabaya, Mataifa yanapaswa kuimarisha ufadhili na utekelezaji wa hatua za kusaidia mataifa na jamii zilizo hatarini zaidi kukabiliana na mapigo ya tabia nchi, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).

Hali hii inaonesha kukabiliana na hali kunapaswa kupewa kipaumbele, ikijumuisha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani, ripoti inaonyesha. Hata hivyo, kwa kuwa uwekezaji kabambe katika kukabiliana na hali hii hauwezi kuzuia kikamilifu athari za mabadiliko ya tabianchi, hasara na uharibifu lazima vishughulikiwe ipasavyo.

Wakizungumza baadhi ya wafugaji akiwemo Jonas Olemeidim amesema Mabadiliko ya tabia ya nchi yamekuwa chanzo Cha umaskini kwao kutokana na Mifugo kukosa malisho na maji. Hali ambayo imesababisha wao kuendelea kuishi kwa kuhamahama kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa ajili ya kutafuta malisho.

Olemeidim amesema chanzo cha Mabadiliko hayo ni kutokana na wingi wa mifugo pamoja na mmomonyoko wa ardhi. Hali ambayo imekuwa desturi kwao kuhamahama kufuata malisho na maji na muda mwingine mifugo kufa njiani kutokana na kutohimili ukame (njaa) wakati wa kuhama, pamoja na maeneo ya malisho na kilimo kutotenganishwa na kusababisha migogoro baina yao na wakulima.

Kwa upande wake, mfugaji mwingine Ndugu Sirya Lesiani amesema mbali tu na mabadiliko ya tabia ya nchi yalivyoadhiri ufugaji, lakini pia ukosefu wa Elimu juu ya ufugaji bora ni changamoto kwao kwani bado  mila na mfumo dume inawakandamiza katika kupunguza idadi ya mifugo.

“Mimi Ng'ombe wangu watano wamekufa kwa sababu ya kukosa chakula, hadi imefika mahali nashindwa kulipa ada ya watoto kwa sababu uchumi wangu ni mifugo sasa kama wamekufa napata wapi pesa? Halafu mwisho wa siku tunapambana kutafuta kwa jasho lakini ukame ukija wanafyeka yote unabaki unashika tama” amesema Sirya Lesian
 
Olemeijo ni kiongozi wa Mila (Alaigwanani) kutoka ukoo wa Mollel. yeye amesema ni kweli wafugaji wanaumia na ukame kwa sababu ya kupoteza mifugo yao kwa wingi, huku akiomba serikali kuongeza nguvu katika kutoa Elimu ya ufugaji Bora. Hii itasaidia kipindi cha ukame mifugo yao isipukutike na kusisitiza Sheria ya utunzaji wa Mazingira kuzingatiwa pamoja na maeneo ya malisho yaliyotengwa.

Kwa Upande wake Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mheshimiwa Fredrick Lowassa amekuwa akitumia majukwaa mbalimbali kueleza juu ya Athari za Mabadiliko ya Tabia ya nchi na kuwaomba wazazi kupunguza wingi wa Mifugo kwani ndio njia pekee ya kukabiliana na hali hiyo, na kusisitiza pia Elimu kwa watoto hususani wa kike na kuwaasa jamii hiyo kuacha kusujudia wingi wa mifugo.

"Ni ukweli usiopingika kuwa kwa sasa hali ni mbaya kwa Wafugaji. Mifugo inapotea kwa sababu ya njaa na kiu. Lakini tunapaswa kufahamu kuwa hili ni janga la Dunia nzima, njia pekee ya kuokoa mifugo yetu kwanza tupande miti, tukipanda miti mvua inanyesha, mvua ikinyesha tunapata majani kwa ajili ya malisho ya mifugo yetu na maji. Pia baada ya mifugo yetu kushiba tunauwezo wa kupeleka sokoni kwa sababu wamepata afya nzuri. Hizo pesa tunawekeza kwenye vitu vingine jamani, tuache kuamini kuwa wingi wa mifugo ndo maisha kwetu, tupandeni miti” amesema Fredrick Lowassa

Kwa upande wao, wafugaji nao wanasema kuwa njia pekee ya kukabiliana na ukame au mabadiliko ya tabia ya nchi ni upandaji wa miti kwa wingi, utunzaji wa mazingira, utunzaji wa maeneo ya malisho na kuomba serikali kuwatengea sehemu za malisho na sehemu za kilimo kwani hata migogoro mingi imekuwa ikitokea baina yao na wakulima, nakuomba Sheria iwekwe na ifuatwe kwa yeyote atakayekaidi sheria hizo.

Pia wameongeza kwa kusema kuwa Serikali ifanye jitihada kuwafikia wafugaji vijijini na sio mijini kwani wanaopata hasara zaidi ni wafugaji vijijini, kwani mafunzo yanayotolewa na serikali na baadhi za taasisi wanaishia mijini na muda mwingine wanawachukua wawakilishi wetu ambao hata hawahusiki na ufugaji na mwisho wa siku mafunzo waliopewa hayatufikii huku vijijini.

Joshua Nassari ni mkuu wa Wilaya hiyo ya Monduli, nae amesema afya ya mifugo na malisho sambamba na maji, ili haya yote yapatikane ni lazima tuheshimu maeneo ya Malisho, Tupande miti kwa wingi lakini pia kupunguza idadi ya mifugo, na  kusema  wakati wananchi wanataka kuboreshewa maeneo hayo yote wahakikishe pia watoto wanaenda shule kwani elimu hii hazina yetu ya baadaye.

Mwanzoni mwa mwaka huu aliyekuwa Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi , ambaye kwa sasa ni Waziri wa Wizara hiyo alifanya ziara Wilayani humo na kukagua eneo la Mnada wa ng'ombe Meserani Duka bovu na kufanya mkutano wa hadhara katika kata ya Naalarami.  Katika Ziara hiyo, Waziri pia alikagua Ujenzi wa Bwawa linalojengwa katika eneo na alisisitiza Wafugaji hao kuheshimu na kutunza maeneo ya Malisho.

"Wakati nakuja nilipitia soko /Mnada wa ng'ombe hapo Dukabovu Meserani kwanza nimesikitika kwa sababu mifugo Haina Afya nzuri kama inavyotakiwa na hii ni kutokana na wingi wa mifugo, mnashindwa kufuga kisasa hivi unajisikiaje leo ukihitaji millioni Moja ni hadi uuze Ng'ombe wanne Hadi watano? Kwanini tusifuge kisasa unafuga mifugo wachache ambao hata ukiamua kuuza dume Moja hata ukitamka millioni Moja au mbili mtu anasema ndiyo ni sawa, tusipobadilika Ukame utatubadilisha manake ukame utavuna mifugo yetu yote, tubadilike wapendwa tutunze mazingira, tupande miti tufuge kisasa, kibiashara zaidi, hata ukiwa na madume Yako kumi au ishirini una uhakika kwamba nikimchukua mmoja itakutatulia shida ulionayo tuwafuge kisasa ili tupate thamani ya mifugo yetu".

Kwingineko duniani, juhudi mbalimbali zimekuwa zikiendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Kwa mfano; Nchini Kenya, Serikali imeanzisha mradi wa "Kenya Livestock Insurance Program" ambao unatoa bima ya mifugo kwa wafugaji ili kuwalinda dhidi ya hasara za kiuchumi kutokana na vifo vya mifugo kutokana na ukame, mafuriko au magonjwa ya mifugo. Kwa upande wake, serikali ya India imeanzisha mpango wa "National Livestock Mission" ambao unalenga kuongeza uzalishaji wa mifugo, kuongeza thamani ya bidhaa za mifugo, na kuboresha afya ya mifugo. Pia, Serikali inasaidia wafugaji katika kupata maji, chakula na huduma za matibabu kwa ajili ya mifugo yao.
Share To:

Post A Comment: