Katibu Mkoa Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu amewataka Watendaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo inakamilika  ndani ya muda uliopangwa ili kuweka rekodi ya kukamilisha miradi ndani ya muda uliowekwa bila kuathiri viwango vya ubora unaokubalika.

Rai hiyo imetolewa Wilayani Kondoa katika kikao kazi baina yake na watumishi wa Halmashauri ya Mji Kondoa huku akihimiza weledi, uzalendo na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kwa kufuata Sheria, Taratibu na Kanuni za Utumishi wa Umma.

"Suala la maadili na weledi katika taaluma zetu ni muhimu sana na nitoe rai kwenu mjitume zaidi, tumieni fursa za uwekezaji na kuendelea kuwaelimisha wengineni ili Mkoa wa Dodoma uendelee kuwa fahari ya watanzania wote" Gugu amefafanua.

Amesema watumishi wana jukumu la kusimamia agenda ya Serikali ya kuhakikisha mipango iliyowekwa inatekelezwa kwa ufanisi katika ngazi zote huku akiangazia suala la hifadhi na usimamizi wa mazingira na kuwataka kuzingatia maelekezo ya Serikali na kutekeleza kwa vitendo Kampeni ya kukijanisha Dodoma.

“Simameni katika nafasi zenu, ili kwa pamoja mtimize malengo mliyojiwekea ya kujiletea maendeleo binafsi na taifa kwa ujumla. Natoa rai kila mmoja kusimama katika  nafasi yake katika kutimiza malengo na majukumu ya msingi. Wekeni utaratibu wa kutatua changamoto zenu kwa njia ya mazungumzo, ikiwa ni pamoja na kukwamua utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wakati, hatutakubali miradi kutokamilika na kuvuka mwaka ifikapo tarehe 30 Juni 2023.

Halmashauri ya Mji Kondoa ni moja kati ya Halmashauri 8 zilizopo katika Mkoa wa Dodoma na ilianzishwa mwaka 2015 ikiwa ni ukubwa wa kilometa za mraba 703 na ipo katika Kata ya Chemchem, Mtaa wa Kwapakacha.

Share To:

Post A Comment: