Na John Walter-Manyara

Imeelezwa kuwa mtindo mbaya wa Maisha, chumvi nyingi kwenye chakula, sukari nyingi na mafuta ni chanzo cha magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwe Shinikizo la juu la damu.

Akizungumza kwenye hafla ya maadhimisho ya siku ya   shinikizo la juu la damu duniani iliyofanyika kitaifa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara, Kaimu Mkurugenzi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara Daktari Yesige Mutajwaa ameeleza kuwa kwa mwaka 2017 idadi ya wagonjwa wa magonjwa yasioyoambukiza waliotibiwa kwenye vituo mbalimbali vya afya nchi ilikuwa ni 2,535,281 na hadi kufikia mwaka wa 2021 idadi ya wagonjwa imeongezeka na kufikia wagonjwa 3,440,708 ambayo ni sawa na ongezeko la silimia 9 la wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza hapa nchini Tanzania.

Kutokana na idadi hiyo ugonjwa wa shinikizo la juu la damu umeonekana kuwa na idadi kubwa ya watu ikilinganishwa na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza kwani kwa mwaka 2017 idadi ya wagonjwa wa shinikizo la juu la damu ilikuwa ni 688,901 na mwaka 2021 idadi iliongezeka na kufikia 1,345,847 huku kwa mwaka wa 2022 ilifikia jumla ya idadi ya wagonjwa 1,456,881.

Aidha kwa utafiti uliofanywa kwenye mikoa ya Pwani, Arusha, Geita, Mtwara, Lindi, Iringa, Zanzibar na Dar es salaam umeonesha kuwa  watu watatu hadi wanne kati ya watu kumi wanashinikizo la juu la damu.

Ugonjwa huu husababisha tatizo la kiharusi, shambulio la moyo na moyo kushindwa kufanya kazi hali inayoweza kupelekea kifo.

Ametoa wito juu ya watu kutunza ikiwemo kula chakula chenye chumvi  na mafuta kiasi na kufanya mazoezi ya mwili ili kupunguza uwezekano wa kupata ugonjwa wa shinikizo la juu la damu ugonjwa ambao umeonekana kuleta athari kubwa kwani maambukizi yameongezeka kwa kasi ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.

 

Kwa upande wake mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza kutoka wizara ya afya Daktari Anzibert Rugakingira  amesema kwa sasa wizara ya afya ipo mstari wa mbele ili kuhakikisha wanachi wanajua namba zao za shinikizo la damu inayosaidia kubaini kwa urahisi tatizo hilo na kuanza matibau mapema kabla tatizo halijaongezeka.

“Ukiwa na shinikizo la juu la damu unaweza usione dalili yeyote, kwahiyo unaweza ukawa unajihisi vizuri kabisa lakini ukienda kupima unakutwa na shinikizo la juu la damu kwahyo kupima ndio njia sahihi ya kuweza kujitambua lakini lazima tujue namna ya kutatua matatizo yetu bila kupata msongo wa mawazo kwani unachangia kupata shinikizo la juu la dmu.”

Siku ya shinikizo la juu damu duniani inakwenda na kauli mbiu isemayo “pima shinikizo lako la damu kwa usahihi lidhibiti ili uweze kuishi maisha marefu’ na kitaifa siku hii imeadhimishwa ndani ya mkoa wa Manyara kwenye viwanja vya hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara na mgeni rasmi wa maadhimisho hayo alikuwa ni mkurugenzi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara Daktari Yesige Mutajwaa.

Siku hii huadhimishwa kila tarehe 17 ya mwezi Mei 5 ya kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha watu kupima afya zao ili kugundua mapema changamoto walizonazo hasa magonjwa yasiyoambukiza na kuweza kufanyiwa matibabu kwa haraka zaidi.

Pia ina lengo la kusisitiza mabadiliko ya mitindo ya maisha ambayo kwa kiasi kikubwa imeonekana kusababisha tatizo la shinikizo la juu la damu ikiwemo kutokufanya mazoezi, kula vyakula vyenye mafuta mengi pamoja na chumvi nyingi na kujenga tabia ya kuchunguza afya mara kwa mara.

 

Share To:

Post A Comment: