Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ameiagiza Wizara ya Nishati kuendelea kusimamia kikamilifu mradi wa usambazaji umeme vijiji (REA) ili uweze kuwa mkombozi kwa wananchi wa hali ya chini hususani wale wa vijijini.

Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 17 Mei 2023 wakati akizindua mradi wa usambazaji wa umeme vijijini (REA) Awamu ya Tatu katika eneo la Sale Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha. Amesema vijana wengi wanaozaliwa katika familia duni wanashindwa kufikia ndoto zao kutokana na kukosa huduma muhimu kama vile nishati.

Makamu wa Rais amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuhakikisha huduma muhimu za jamii zinawafikia wananchi ili waweze kufikia maendeleo kwa haraka zaidi. Pia ameitaka TANESCO Wilaya ya Ngorongoro kutoa elimu kwa wananchi ili kukabiliana na  vishoka na kuhakikisha wanavijiji wanapata huduma ya umeme kwa bei ya ruzuku kama iliyopangwa na serikali.

Aidha Makamu wa Rais akiwa katika nyumba ya mfano iliopokea huduma ya umeme wa REA ya Mama Gladness Gilole iliopo Sale Wilayani Ngorongoro amesema serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais itamuwezesha Mama huyo kusomesha watoto wake wawili hadi kidato cha nne kutokana na maombi ya mama huyo mjane anayekabiliwa na changamoto mbalimbali.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato amesema serikali imeendelea kutoa ruzuku katika kuwaunganishia wananchi umeme maeneo ya mijini na vijijini kwa kupunguza gharama halisi za kuunganisha umeme ikiwemo kutoza shilingi elfu 27 kwa maeneo ya vijijini ikiwa gharama halisi ni zaidi ya laki nane.

 Ameongeza kwamba mradi wa umeme vijijini unakwenda sambammba na utolewaji wa kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) ambacho kinawasaidia wananchi kuunganisha umeme kirahisi kwa wale wenye kipato kidogo wanaoshindwa kuweka mfumo wa upokeaji umeme (Wiring) katika nyumba zao.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amezindua mradi wa barabara ya Mto wa Mbu - Loliondo sehemu ya Wasso – Sale yenye urefu wa kilometa 49, hafla iliofanyika katika eneo la Sale Wilaya ya Ngorongoro.

Akizungumza na wananchi mara baada ya kuzindua barabara hiyo, Makamu wa Rais ametoa wito kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kutoa kipaumbele cha pekee kwa ujenzi wa barabara kiwango cha lami eneo la Ngaresero -Engaruka ambalo limekuwa changamoto kubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro kwa muda mrefu.

Pia Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Ardhi kushughulikia mgogoro wa mashamba uliopo katika eneo la Sale pamoja na kutoa wito kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Maliasili na Utalii kushughulikia vema suala la eneo la malisho ya mifugo kwa wananchi wa Ngorongoro ili kuhakikisha kunakuwa na mipaka yenye kuzingatia uendelevu wa watu na mali zao.

Halikadhalika Dkt. Mpango amewahimiza wananchi wa Ngorongoro kuhakikisha wanatunza mazingira kama njia ya  kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na usalama wa chakula cha mifugo ambao umewafanya wakazi wa maeneo hayo kuishi kwa kuhamahama. Amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro kuanzisha kampeni maalumu ya upandaji miti katika wilaya hiyo na kufanya jambo hilo kuwa la lazima kwa wananchi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema ufunguzi wa barabara hiyo ni kudhihirisha kwa vitendo lengo la serikali ya awamu ya sita ya kuunganisha wilaya zote na makao makuu ya mikoa ambapo wizara imeweka dhamira ya kuhakikisha iifikapo 2025 wilaya zote zinaunganishwa kwa barabara za kiwango cha lami na makao makuu ya mikoa.

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara nchini TANROAD mhandisi Rogatus Mativila amesema kusudio la ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ni kupunguza adha ya usafiri pamoja na muda wa usafirishaji wa mazao na mifugo kutoka ukanda huo, hususani kwa wakazi wa Ngorongoro katika mji wa Loliondo na vitongoji vyake. Ameongeza kwamba barabara hiyo itachochea ukuaji wa sekta ya utalii katika taifa pamoja na kuongeza thamani ya mazao na mifugo hivyo kukuza kipato kwa wananchi waishio maeneo hayo.

Ujenzi wa Barabara ya Mto wa Mbu – Loliondo wenye jumla ya kilometa 217 umegawanywa katika sehemu nne ambazo ni Wasso – Sale (Km49) Sale – Ngaresero (Km 57.4) Ngaresero -Engaruka (Km 39.2) pamoja na Engaruka – Mto wa Mbu (Km 60) ambapo utaekelezaji wa ujenzi ulianza kwa sehemu ya Wasso – Sale ambayo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100.

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Arusha ambapo anakagua shughuli za maendeleo, miradi pamoja na kusikiliza kero za wananchi.












Share To:

Post A Comment: