BUTIAMA-MARA


Ikiwa kila Aprili 13 ni siku ya kuzaliwa kwa aliyekuwa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Taasisi ya Mwalimu Nyerere leo imezindua wiki ya kumbukizi ya Hayati Mwalimu Nyerere ili kuhuisha falsafa ya maisha yake na kuhakikisha maisha aliyoyaishi yanaendelezwa na kuenziwa kwa manufaa ya ustawi wa jamii na Nchi, uzinduzi uliofanyika Mwitongo Wilayani Butiama.


Akifungua wiki ya kumbukizi hiyo Naibu Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Butiama ambapo ndipo alipozaliwa Hayati Baba wa Taifa, Mhe. Jumanne Sagini amesema kuwa falsafa za Mwalimu Nyerere kwetu sisi Watanzania zilienzi katika kutetea Uhuru, Umoja, Kujitegemea, Haki, Utu, Heshima kwa binadamu, Usawa na Demokrasia kwa kuwa muumini asiyetetereka katika misingi hiyo kwa hapa nchini lakini pia katika siasa za dunia jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa katika taswira ya Nchi ya Tanzania tunayoiona sasa.


“Msingi wa fikra na falsafa za Mwalimu Nyerere ulijengeka hapa Butiama. Jambo linaloleta faraja ni kwamba fikra na maono mbalimbali ya Babab wa Taifa yametambuliwa na kutekelezwa na awamu zote za Uongozi wa Nchi yetu. Maono ya Msingi ikiwemo Umoja wa Taifa, Maendeleo ya Taifa,dhana ya kujitegemea,dhana ya kujituma kufanya kazi vilikuwa ni vitu ambavyo vimethaminiwa na kuendelezwa ikiwa ni sambamba na ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati na kuhakikisha Mtanzania anakombolewa kielimu na kiuchumi.”alisema Sagini


Katika hatua nyingine Naibu Waziri Sagini amewataka Wazazi kuendelea kusimamia na kutekeleza wajibu wa malezi ya Watoto ili kuendelea kusimamia maadili ya Taifa na kwa kuzingatia Mila, Desturi na Tamaduni tulizorithishwa na Waasisi wa Taifa akiwemo Hayati Mwalimu Nyerere.


Awali akizungumza katika Uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Profesa Francis Matambalya amesema kuwa licha ya kuwa na siku ya kumbukizi ya Kifo cha Hayati Mwalimu Nyerere ambayo huadhimishwa ifikapo 14 Oktoba ya kila mwaka siku hiyo imekuwa na shughuli nyingi za Kitaifa ikiwemo kuzima mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa na hivyo kuamua kuja na wiki ya kumbukizi ili kuweza kutoa elimu zaidi kwa jamii.Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: