Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma Micheal Mbano kushoto akimuongoza mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za serikali za mitaa(LAAC)Mheshimiwa Halima Mdee katikati kwenda kukagua vikundi vya wajasiriamali eneo la Lilambo.

 KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya serikali za mitaa(LAAC),imenusa harufu ya ufisadi kwenye fedha za mikopo ya asilimia kumi inayotolewa kwa vikundi vya vijana,wanawake na walemavu katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.


Kamati hiyo imebaini upotevu wa zaidi ya Sh.milioni 203,kati ya hizo Sh.milioni 134 zilizotengwa kama mikopo kwa vikundi maalum vya wanawake,vijana na walemavu,Sh.milioni 32 za madawati na Sh.milioni 37 kwa ajili ya kuchangia miradi ya maendeleo lakini hazikufanya kazi iliyokusudiwa.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Halima Mdee,wakati akizungumza na watumishi na wataalam wa Manispaa hiyo mara baada ya kamati kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Manispaa ya Songea.

Mdee alifafanua kuwa,kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo wa vikundi vya vijana,wanawake na walemavu ya mwaka 2009 inataka kila Halmashauri kuchangia asilimia 10 ya mapato yake ya ndani yasiyolindwa katika mfuko huo.

Alisema, kwa mwaka wa fedha 2020/2021 Menejimenti ya Manispaa ya Songea ilitoa Sh.milioni 137 tu,badala ya Sh.321 ambayo ndiyo iliyokuwa asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa mwaka huo huku kiasi cha Sh.milioni 134 zilizobaki hazifahamiki zimekwenda wapi.

Mdee alieleza kuwa, kwa ujumla mwenendo wa utoaji wa mikopo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ulikuwa mbovu ambapo vikundi vilipewa fedha bila kuwa na ufumbuzi yakinifu wa biashara zilizokuwa zinafanyika.

Alisema, hata katika Daftari la kumbukumbu la mikopo la mfuko wa vikundi vya vijana,wanawake na walemavu lilionyesha kuwa vikundi 80 vilivyopewa mikopo ya Sh.milioni 95.6 vimekufa,havipo na haviwezi kurudisha mkopo huo.

Lakini,baada ya ofisi ya CAG kukagua na kufuatilia nyaraka mbalimbali ilibaini vikundi 55 kati ya 80 vipo na vinaendelea kufanya kazi ambapo viliweza kurudisha kiasi cha Sh.milioni 30.2.

Alisema,katika mwaka wa fedha 2020/2021 Manispaa ya Songea imeshindwa kutenga asilimia 40 ya mapato yake ya ndani yasiyolindwa ambayo ni Sh.milioni 128 kwenye miradi ya maendeleo, badala yake ilitoa Sh.milioni 124 na kiasi cha Sh.milioni 37 hazikutolewa na hazijulikani zilipo.

Aidha,kwa mwaka wa fedha 2020/2021 Menejimenti ya Manispaa ya Songea ilidai kutumia Sh.milioni 32.6 kununua mbao kwa ajili ya kutengeneza madawati katika shule ya msingi Mitendewawa na Misufuni,lakini baada ya CAG kufuatilia alibaini kuwa shule hizo hazikupata madawati hayo.

Mdee ameitaja Manispaa ya Songea imekithiri kwa kutozingatia na kufuata miongozo mbalimbali ya serikali na kutoa taarifa za uongo kwa ofisi ya Mkaguzi na mdhibiti Mkuu wa Hesabu za serikali(CAG)kwa mwaka wa fedha 2020/2021.

Kwa mujibu wa Mdee,kifungu cha 15 cha sheria ya ukaguzi wa umma cha mwaka 2014 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2020 kinazitaka taasisi za umma kumpatia mkaguzi wa ndani(CAG)taarifa zote muhimu anazozihitaji kwa ajili ya utekelezaji wa kazi zake.

Mdee alisema,Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea amekiri katika maeneo mbalimbali taarifa yake imetofautiana na taarifa ya CAG kwa kamati kwa sababu ameshindwa kumpatia CAG taarifa zote muhimu anazozihitaji jambo ambalo ni kosa na kumtaka Mkurugenzi kuheshimu kazi za CAG.

Pia alisema,kwa mwaka wa fedha 2020/2021 Manispaa ya Songea ilijenga vyumba vya madarasa katika maeneo mbalimbali,hata hivyo badala ya kujenga kutokana na miongozo ya serikali kwa kufuata taratibu za manunuzi(BOQ) Manispaa hiyo ilifanya mabadiliko bila kuwasiliana na ofisi ya Rais Tamisemi.

“kazi iliyofanyika katika ujenzi wa mradi wa bwalo la chakula katika shule ya sekondari Dkt Emmanuel Nchimbi ni nzuri,tumeona kazi ni nzuri ingawa imefanyika kinyume na utaratibu uliowekwa na wizara husika,tunajua mkaguzi mkuu atapita kukagua na kujiridhisha juu ya ongezeko la Sh.milioni 65 zilizotumika katika ujenzi huo”alisema Mdee.

Alisema,utendaji wa watumishi katika Manispaa ya Songea kurekebishwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu.

Mwenyekiti huyo wa kamati ya kudumu ya Bunge,ameiagiza ofisi ya katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma,kudhibiti Halmashauri zake juu ya matumizi mabaya ya fedha na kuwachukulia hatua kali watumishi wanaokwamisha juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Tamisemi anayeshughulikia Afya Dkt Wilson Mahera,amehaidi ofisi yake kufanyia kazi ushauri uliotolewa na kamati hiyo ili kuleta tija,ufanisi na kutoa huduma bora kwa Watanzania.

Dkt Mahera amewataka watumishi wa Manispaa ya Songea,kubadilika kiutendaji na kufanya kazi kwa kufuata sheria,kanuni,weledi,uaminifu na kuzingatia miongozo mbalimbali ya serikali na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michela Mbano alisema, watayafanyika kazi mapungufu yaliyojitokeza na kuhakikisha kuwachukulia hatua watumishi waliosababisha kuzalisha hoja za CAG.

Kamati hiyo imefanikiwa kupita na kukagua jumla ya miradi mitatu ya ujenzi wa bwalo la chakula katika shule ya sekondari Dkt Emmanuel Nchimbi,ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika shule ya msingi Mitendewawa na eneo la viwanda katika kata ya Lilambo.
 Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za serikali za mitaa(LAAC)Mheshimiwa Halima Mdee kushoto,akimsikiliza kaimu Mhandisi wa ujenzi wa Manispaa ya Songea Nichlous Danda baada ya kutembelea ujenzi wa mradi wa Bwalo la chakula katika shule ya sekondari Dkt Emmanuel Nchimbi.

 Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge la Hesabu za serikali za mitaa(LAAC)Mheshimiwa Halima Mdee kushoto akiangalia asali inayouzwa na kikundi cha wajasiriamali wadogo waliopata mkopo wa fedha kutoka Halmashauri ya Manispaa ya  Songea mkoani Ruvuma.
Share To:

Post A Comment: