Na John Walter-Manyara

Jeshi la Polisi mkoani Manyara limesema limeweka mikakati kabambe  kudumisha hali ya usalama wakati wa siku kuu ya Iddi.

Mikakati hiyo inalenga kukabiliana na aina yoyote ya uhalifu katika mitaa na vijiji katika mkoa huo wenye wilaya tano.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoani hapa George Katabazi katika taarifa yake kwa waandishi wa Habari leo April 19,2023 mjini Babati, amewahakikishia wakazi wa mkoa huo kuwa siku kuu hiyo itafanyika kwa amani na utulivu.

Amesema wataongeza doria na Misako maeneo yote, kwenye bara bara kuu na  nyumba za ibada.

Hata hivyo Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) limetangaza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi katika Baraza la Iddi.

Taarifa ya Katibu Mkuu wa Bakwata Taifa, Nuhu Mruma imeeleza kuwa baraza hilo litafanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere kuanzia saa 8.30 mchana.

Mruma ameeleza kuwa sherehe za Iddi El-Fitri kitaifa zitafanyika katika Mkoa wa Dar es Salaam Aprili 21 au 22 kutegemea mwandamo wa mwezi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, Swala ya Iddi itaswaliwa katika Msikiti wa Mfalme Mohamed VI, Bakwata Makao Makuu Kinondoni kuanzia saa 1.30 asubuhi.

“Kwa niaba ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dk Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally Mbwana anawatakia Waislamu na wananchi wote maandalizi mema ya sikukuu hiyo,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

 

Share To:

Post A Comment: