Na Benny Mwaipaja, Washington D.C, Marekani


BENKI ya Dunia imeimwagia sifa Tanzania kwa usimamizi mzuri wa uchumi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayopata fedha kutoka kwenye taasisi hiyo ikilinganishwa na nchi nyingine nyingi za Afrika.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika (Africa Group 1 Constituency), Dkt. Floribert Ngaruko, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania, unaoongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kwenye Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Jijini Washington D.C, nchini Marekani.

Dkt. Ngaruko, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Benki ya Dunia katika ukanda huo, alisema kuwa Tanzania ni nchi ya mfano katika usimamizi wa sera za uchumi na fedha ambapo licha ya changamoto za UVIKO 19 na vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine, tathimini ya Benki hiyo inaonesha kuwa uchumi wa Tanzania uko imara ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika.

“Tanzania ni nchi ya kupigiwa mfano kwa usimamizi mahili wa masuala ya uchumi mpana, sit u kwa nchi za Afrika Mashariki, bali kwa nchi za Afrika, ambapo kiwango cha ukuaji uchumi cha wastani wa asilimia 5.4 ni cha juu, na ninawapongeza sana” alisema Dkt. Ngaruko

Aidha, alipongeza uhusiano imara uliopo kati ya Tanzania na Benki ya Dunia na kuahidi kuwa Benki yake itaendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za kukuza uchumi na kuwaondolea umasikini wananchi wake kwa kusaidia fedha zitakazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii pamoja na kutoa misaada ya kiufundi.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alimweleza Mkurugenzi huyo Mtendaji wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika, Dkt. Floribert Ngaruko, kwamba uchumi wa Tanzania unazidi kuimarika na kwamba Serikali itaendelea kuchukua hatua muhimu kuhakikisha uchumi unazidi kuimarika na kuleta ahueni kwa wananchi.

Alifafanua kuwa katika kipindi cha robo tatu robo ya mwaka 2022/2023 uchumi umekua kwa asilimia 5.2 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha uliotangulia 2021/2022 na kwamba kutokana na mipango kabambe iliyowekwa na Serikali uchumi utakua zaidi hadi kufikia wastani wa zaidi ya asilimia 6.3 miaka michache ijayo.

Aidha, Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, aliishukuru Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo kwa kuiidhinishia Tanzania dola za Marekani bilioni 1.635 katika mzunguko wa 20 wa IDA (Julai 2022 – Juni 2025) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 6 ya maendeleo katika sekta mbalimbali inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi pamoja na kupunguza umasikini wa wananchi.

“Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi makini wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania, tunaahidi kuwa tutasimamia na tutatumia fedha hizo kwa umakini ili kufikia malengo yaliyokusudiwa” Alisema Dkt. Nchemba

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum, aliishukuru Benki ya Dunia kwa kusaidia ustami na maendeleo ya watu wa Zanzaibar kwa kufadhili miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ikiwemo ya elimu na ujenzi wa miundombinu ya usafiri wa anga.

“Ujenzi wa miundombinu hiyo imekuza sekta ya utalii lakini bado tunachangamoto ya upatikanaji wa nishaji ya umeme wa uhakika na tunaamini tutaendelea kushirikiana na Benki yako kutatua changamoto hiyo na changamoto nyingine zinazotukabili” alisema Dkt. Saada

Mpaka sasa Benki ya Dunia imewekeza zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 7.2, sawa na takriban shilingi za Tanzania trilioni 16.7 kwa ajili ya kutekeleza miradi zaidi ya 29 nchini Tanzania ambapo kati ya miradi hiyo, 24 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 6.41 ni ya kitaifa na mingine 5 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 0.75 ni ya kikanda.

Share To:

Post A Comment: