Na Mwandishi Wetu 

Katika kupambana na udanganyifu unaofanywa na wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wasio waaminifu jumla ya wanachama 468 wa mikoa mbalimbali wamefungiwa uanachama wao kutokana na kubainika na matumizi mabaya ya kadi zao.

Aidha wanachama husika walitakiwa kurejesha gharama zote zilizotokana na matumizi ya vitambulisho husika na jumla ya Shilingi  112,625,366.07 zimesharejeshwa.

Haya yako katika taarifa mbalimbali za NHIF zinazoonesha namna Mfuko huo unavyopambana na suala hilo. 

“Ili kuhakikisha mapambano dhidi ya udanganyifu yanaendelea Mfuko unaendelea kuimarisha mifumo ya ndani ya TEHAMA ya uchakataji madai ili kuweza kuzuia na kugundua vitendo vya udanganyifu mapema pamoja na kushirikiana na vyombo vingine vya dola kama Polisi na TAKUKURU,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Mfuko umekuwa ukifanya chunguzi mbalimbali kwa watoa huduma, waajiri, wanachama na watumishi wa ndani ambapo kwa upande wa Watumishi jumla ya Watumishi 17 wa Mfuko walifukuzwa na kazi kutokana na kushiriki vitendo hivyo.

Akizungumzia suala hili Meneja wa Kitengo cha Kudhibiti Udanganyifu cha Mfuko Dk. Rose Ntundu amesema, ni moja ya majukumu ya Mfuko kudhibiti udanganyifu na Mfuko unachukua hatua kwa wanaobainika ikiwa ni pamoja na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Share To:

Post A Comment: