Na Joachim Nyambo,Mbeya.

 TAASISI ya WeCare kwa kushirikiana na Hospitali ya Aghakhan wamefungua kituo cha Maendeleo ya awali ya mtoto kitakachotumika kutoa mafunzo kwa wazazi na walezi wa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano juu ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(MMMAM) hospitalini hapo.

Kuanzishwa kwa kituo hicho ni sehemu ya Taasisi binafsi kuunga mkono juhudi za serikali kwenye utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Kitaifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) inayoendelea kutekelezwa katika mikoa kumi nchini ukiwemo Mkoa wa Mbeya.

Akimwakilisha Mganga Mkuu wa Jiji la Mbeya,Dk Jonas Lulandala kuzindua kituo hicho,Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto jijini hapa, Aquina Mtweve alipongeza hatua ya taasisi hizo kuamua kuwekeza kwenye ukuaji wa awali wa mtoto hatua aliyosema inalenga kuwezesha kuwa na taifa lililo na rasilimali watu walio na ukuaji timilifu hapo baadaye.

Mtweve aliwataka wazazi na walezi kutambua kuwa kinachofanywa na serikali na wadau katika kusimamia ukuaji sahihi wa mtoto si maigizo bali kuna faida kubwa hivyo ni muhimu kwao wakawa tayari kupokea yale yanachofundishwa na wataalamu na kuyafanyia kazi majumbani.

“Tumeona hapa mwalimu alipotuonesha namna ya uchangamshaji watoto kupitia michezo… unaweza ukaona kama ni maigizo au ni mchezomchezo tu…lakini huu ndiyo msingi muhimu sana wa ukuaji wa mtoto… Wazazi na walezi haya ndiyo tunapaswa kuyafanya majumbani ili kuwajenga watoto kuwa na ukuaji timilifu.” Alisisitiza Mtweve.

 “Tunafurahi kuona kituo hiki ambacho ni cha kwanza hapa mkoani kwetu kinafunguliwa katika jiji letu. Tunajua kwamba katika Mkoa wa Mbeya, jiji ndilo linabeba idadi kubwa ya wakazi hivyo tukifanikisha hapa tutafanikiwa kimkoa pia.” Aliongeza.

 Hata hivyo Mratibu huyo wa Afya ya Uzazi na mtoto alishauri Taasisi husika na wadau wengine kuona uwezekano wa kufungua vituo vingine kama hivyo kwakuwa uhitaji ni mkubwa.

 Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Tasisi ya WeCare, Elizabeth Magunga alisema walifikia uamuzi wa kufungua kituo hicho baada ya kuona watoto waliokuwa wakiwapokea kwenye kituo chao cha malezi ya awali ya mchana wakiwa na mapungufu mbalimbali ya ukuaji kutokana na wazazi kukosa uelewa wa kutosha juu ya namna sahihi ya kumsaidia mtoto kupitia ukuaji timilifu.

Magunga alisema kupitia kituo hicho sasa wazazi watakao kuwa wakihudhuria kliniki katika Hospitali ya Aghakan na wale watakao fika siku atakazopanga daktari wa watoto hospitalini hapo watapata wasaa wa kukutana na kujifunza kutoka kwa wataalamu wa MMMAM.

Aliyataja maeneo makuu matano yatakayozingatiwa kwenye utoaji elimu kwa wazazi kupitia kituo hicho kuwa ni pamoja na Afya, Lishe bora, Malezi yenye muitikio, Ulinzi na Usalama pamoja na Ujifunzaji wa awali.

Naye Meneja wa Hospitali ya Aghakhan tawi la Mbeya,Michael Mwanisenga alisema uwepo wa kituo hicho utaisaidia pia jamii kuondokana na baadhi ya maradhi yanayowakabili watoto yanayotokana na wazazi na walezi kukosa uelewa wa kutosha wa namna ya kuwakinga watoto wao ikiwemo udumavu na utapiamlo.

 Mwanisenga aliwakaribisha wadau wengine walio na utayari wa kushirikiana na hospitali hiyo kwenye uwekezaji unaoweza kuisaidia jamii akisema lengo ni kuona kunakuwa na ustawi kwenye jamii kwa kuepuka maradhi hususani yanayohatarisha maisha ya watoto.

 

Share To:

Post A Comment: