Na;Elizabeth Paulo, Dodoma

Katika kukuza  uwekezaji wa  shughuli za usafiri majini na uvuvi, Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wakala wa Meli Tanzania TASAC inaendelea kukamilisha Mradi wa Kimataifa wa Mawasiliano na Uchukuzi katika Ziwa Victoria (Multi-National Lake Victoria Maritime Communication and Transport  MLVMCT).


Pamoja na malengo mengine Lengo la mradi huo ni pamoja na kujenga vituo vinne (4)  vya uokozi (search and rescue centres-(SARs)) ambavyo vitakuwa kimoja kimoja katika maeneo ya Kanyala  Sengerema, Musoma - Mara, Nansio - Ukerewe na Ilemela  Mwanza .


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Bw. Kaimu Abdi Mkeyenge Ameyasema hayo wakati akieleza utekelezaji wa Shirika hilo katika Mkutano wa Waandishi wa Habari Uliofanyika leo  Machi 3, 2023 Jijini Dodoma Katika Ukumbi wa Idaya ya Habari Maelezo.


Bw. Mkeyenge amesema Vituo hivyo vitasaidia katika kushughulikia changamoto za usafiri kwa njia maji na katika uokozi majini, kuimarisha usalama wa vyombo vya usafiri kwa njia maji na kuongeza fursa za kiuchumi kwa jamii zinazoishi kandokando ya Ziwa Victoria. Mradi huo unatekelezwa na nchi za Tanzania na Uganda kwa kugharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 59.23 ambapo upande wa Tanzania gharama za mradi ni Shilingi Bilioni 19.97 zinazojumuisha gharama za kazi za ndani na sehemu ya mchango wa Tanzania katika kugharamia kazi za kikanda zinazofanywa kwa kushirikiana na Uganda. 


Aidha  Mradi wa Kimataifa wa Mawasiliano na Uchukuzi katika Ziwa Victoria unatarajiwa kukamilika mnano mwezi Desemba, 2024 na tayari Mshauri Elekezi ameshakabidhiwa maeneo ya kufanyia kazi. 


Katika hatua nyingine Shirika limeshiriki kuongeza mchango katika Mfuko Mkuu wa Serikali mwaka hadi mwaka kutoka Shilingi Bilioni 9.1 katika mwaka wa fedha 2018/19 hadi kufikia Shilingi Bilioni 43.5 katika mwaka wa fedha 2021/22 sawa na ongezeko la asilimia 21 na hivyo kufanya jumla ya mchango wa TASAC katika mfuko mkuu wa Serikali kwa kipindi cha miaka minne kuwa Shilingi Bilioni 104.5.


Amesema katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita, TASAC tangu kuanzishwa kwake 2019 inajivunia  juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya usafiri majini ikiwa ni pamoja na Kukagua meli za nje zinazofika katika bandari zetu 


“kwa mujibu wa Makubaliano ya nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi (Indian Ocean Memorandum of Understanding – IOMOU) ambayo Tanzania ni mwanachama,Katika utekelezaji wa hili TASAC tumekagua meli za kigeni 36 kwa kipindi kuanzia julai 2022 hadi desemba 2022, na kuanzia Januari 2023 tumekagua meli za kigeni 37 ambapo tunategemea kukagua meli 61 hadi kufikia juni 2023”.Alisema Mkeyenge


Akiendelea kutaja mafanikio mengine  ndani ya Serikali ya awamu ya Sita Mkurugenzihuyo amesema TASAC imeanza majadiliano ya kuingia katika makubaliano (Memorandum of Understanding  MoUs) ya kutambuliana vyeti vya mabaharia ili kufungua fursa za ajira kwa mabaharia nchini ambapo nchi 19 ikiwemo Panama, Malta, Cyprus, Qatar, Korea, Ghana pamoja na Jamhuri ya Watu wa China. 


“Mazungumzo yapo katika hatua mbalimbali na yanaendelea vizuri kwa baadhi ya nchi kwa mfano Qatar tayari wameshakubali na tunatarajia kuwekeana saini muda wowote kuanzia sasa”Alieleza


Amesema TASAC imewajengea uwezo maafisa 42 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali kuhusu uratibu wa utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Dharura katika kukabiliana na umwagikaji wa mafuta baharini (National Maritime Oil Spill Response Contingency Plan NMOSRCP).


“katika kutekeleza hili TASAC imeendelea kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa wetu, hususan wanaofanya kaguzi kwa vyombo vya kigeni vinavyoingia katika bandari zetu Port State Control (PSC) ambapo kwa kipindi cha kuanzia julai 2022 hadi Februari 2023, maafisa 11 wamepata mafunzo hayo,na kufikia juni 2023 maafisa wengine 6 watapata mafunzo hayo, 3 katika nchi ya Italia na 3 katika nchi ya Bangladeshi”.Alifafanua


Bw. Mkeyenge Ameendelea kusema Sekta ya Usafiri Majini  zinaweza kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi kama vile kwa kuanzisha utaratibu wa kusajili meli kwa masharti nafuu (open registry), kuanzisha maeneo ya ukarabati na ujenzi wa meli katika ukanda wa pwani na kuanzisha maegesho ya boti ndogo katika ukanda wa pwani, kuanzisha viwanda vya utengenezaji malighafi za ujenzi wa boti za plastiki (fibre) pamoja na kujenga bandari rasmi za uvuvi. TASAC imeishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuiwezesha na kuisaidia TASAC ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa huku wakishukuru Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi chini ya Waziri  Mhe. Prof. Makame Mbarawa, kwa kuendelea kusimamia Shirika na kuongoza vyema katika utekelezaji wa majukumu yake.

Zamaradi Kawawa Mkurugenzi msaidizi Idara ya Habari Maelezo  kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Gerson Msigwa ameshukuru Wakala wa Meli Tanzania TASAC kwa kushiriki katika Mkutano huo ambao ni Moja ya mikutano ya mashirika mbalimbali inayoendelea jijini Dodoma Katika ukumbi wa Habari Maelezo 

Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: