Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akitoa taarifa ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha miaka miwili tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani ambapo alipongeza kazi nzuri iliyofanywa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida  kwa kutekeleza miradi 113 ya umeme yenye thamani ya zaidi ya Sh. Bilioni 4.8. 

Na Dotto Mwaibale, Singida

MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, amesema miradi 113 ya umeme yenye thamani ya zaidi ya Sh. Bilioni 4.8 imetekelezwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutumia fedha za ndani.

Serukamba ameyasema hayo jana Machi 18, 2023, mjini hapa, wakati akizungumzia mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Dk.Samia.

“Hali ya upatikanaji umeme ni ya kuridhisha kwa wilaya zote, hadi sasa jumla ya vijiji 318 sawa na asilimia 72.11 kati ya 441 vilivyo sajiliwa vimeunganishwa umeme wa gridi ya taifa,” alisema Serukamba.

Alifafanua kuwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa, linaloongozwa na Meneja wake, Mhandisi Florence Mwakasege, linasimamia miradi mikubwa minne ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kwenye vijiji 123 yenye thamani ya zaidi ya Sh.Bilioni 73.

“Mkoa uliwaunganishia wateja wapya 19,223 wanaojumuisha shule 287, zahanati 75, visima vya maji 23, viwanda vidogo 76, migodi mitano ya madini ya dhahabu, misikiti 43, makanisa 60, mahakama mbili na vituo 102 vya kibiashara,” alisema Serukamba.

Alibainisha kuwa wapo wakandarasi katika vijiji 123 kukiwa na matarajio ya kuwasha vijiji 13 ifikapo Machi 30, 2023 na vingine vilivyo baki ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.

Serukamba alitanabahisha kuwa ujenzi wa njia kuu za kusafirisha umeme msongo wa kilovolti 400 Singida, Namanga jumla ya kilomita 155 zimekamilika ujenzi wake upande wa Singida.

Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida, Mhandisi Florence Mwakasege akiwa katika moja ya matukio ya kikazi hapo alikuwa anazungumza na Wananchi wa Kata ya Iguguno wilayani Mkalama  wakati akisikiliza mahitaji na ushauri wao kuhusu sekta ya nishati ikiwa ni uboreshaji wa huduma za shirika hilo.
Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida, Mhandisi Florence Mwakasege (katikati mbele) akiwa katika picha ya pamoja na Wafanyakazi wa shirika hilo Mkoa wa Singida katika moja ya matukio yao. Ushirikiano wa wafanyakazi hao,  viongozi wao, wananchi na wadau wengine ndio umeleta mafanikio makubwa katika shirika hilo ndani ya miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani.
Baadhi ya Wanawake watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida wakiwa katika picha ya pamoja. Watumishi hawa wanawake pamoja na wenzao wamekuwa chachu kubwa ya ufanyaji kazi uliotukuka kwa kuunga jitihada za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha nishati ya umeme inamfikia kila mwananchi hapa nchini mafanikio ambayo yameonekana katika kipindi cha miaka miwili cha uongozi wake tangu aingie madarakani. 

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: