Baadhi ya wanafunzi wapya wakifurahia maisha yao ya shule mara baada ya kuandikishwa (Picha kwa Hisani ya Mtandao)

Na Abby Nkungu, Singida 

JUMLA ya watoto 54,710 wenye umri usiozidi miaka sita wameandikishwa kuanza  masomo ya awali kwenye shule mbalimbali zilizopo halmashauri za mkoa wa Singida katika kipindi cha Januari hadi Machi 10 mwaka huu ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya elimu.

Taarifa ya idara ya elimu iliyotolewa kwenye kikao cha Kamati ya ushauri ya mkoa wa Singida (RCC) inaonesha kuwa idadi hiyo ya watoto walioandikishwa ni sawa na asilimia 99 ya lengo la kuandikisha watoto 55, 262.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa kati ya walioandikishwa kuanza masomo ya awali, 27,953 ni wavulana na 26,757 ni wasichana ambapo miongoni mwao 58 ni watoto wenye mahitaji maalumu.

Imeelezwa kuwa Wilaya ya Ikungi ndiyo inayoongoza kwa kuandikisha watoto 12,076, ikifuatiwa na Wilaya ya Singida  watoto 11,060, Mkalama (7,919), Iramba (7,868), Manispaa ya Singida (6,378), Manyoni (4,597) na Itigi watoto 4,812.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Singida, Elia Digha alisema kuwa idadi kubwa ya watoto walioandikishwa mwaka huu inaonesha kuwa jamii imeanza kuelewa na kutambua kuwa elimu ya awali ni muhimu katika kumuandaa mtoto kuanza darasa la kwanza.

“Ukiangalia makadirio yalikuwa kuandikisha zaidi ya watoto 55,000 lakini tumefikia  54, 000 ni  hatua nzuri kwa jamii yetu kuanza kuwa na mwitikio mkubwa  wa kuandikisha watoto elimu ya awali” alisema na kuungwa mkono na  Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, James Mkwega ambaye alisema hata kiwango cha ubora wa elimu kinaweza kupanda kwa watoto kuanza kuandaliwa mapema kimasomo kabla ya  kuanza darasa kwa kwanza.

“Ujue yanapokuja matokeo ya darasa la saba mara nyingi unakuta shule za Mjini zinafanya vizuri zaidi kuliko za kwetu Vijijini. Hii ina maana kwamba pamoja na miundombinu, walimu na mengine, lakini wenzetu msingi mkubwa na mzuri unaanzia kwenye chekechea” alisema.

Alifafanua kuwa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto iliyoanza kutekelezwa Januari mwaka 2021 imesadia katika kuleta mwamko huo wa elimu ya awali.

“Programu hii inalenga watoto wa chini ya miaka 8 umri  ambao ndio wa Chekechea, darasa la kwanza au la  pili, na masuala yanayoangaliwa zaidi ni elimu, afya, lishe, ulinzi, usalama na mengine mtambuka.  Kwa hiyo, naweza kusema uandikishaji huu ni sehemu ya mafanikio ya Programu hiyo” alieleza.

Naye Hamisi Ali mkazi wa Sabasaba na  Anna Elia mkazi wa Utemini mjini Singida wanasema, pamoja na mwitikio chanya wa  wazazi na walezi kupeleka watoto wao kuanza masomo ya awali bado kuna haja kwa Serikali kuweka mazingira rafiki kwa kundi hilo kupata elimu.

“Wenzetu wa shule binafsi kuna kitu wanatuzidi.... wana sehemu ya michezo, uji au chai na chakula, mazingira safi pia usafiri. Kwa hiyo, mtoto anavutiwa kwenda shule ila sasa hizi za Serikali baadhi yake hata uji hakuna na kwa mtoto mdogo lishe ni muhimu kumjenga kiakili” anasema  Hamisi na kuungwa mkono na Anna ambaye anataka shule za awali ziboreshwe zaidi kuvutia watoto wadogo.

Tanzania ni nchi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kuifanya elimu ya Awali kuwa ya lazima kwenye Sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 ili kuijumuisha elimu ya Awali katika elimu za Msingi kwa kuzitaka shule zote kuwa na darasa la elimu ya awali kwa watoto wa chini ya miaka mitano. 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, James Mkwega akichangia jambo katika moja ya mkutano mkoani hapa hivi karibuni.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Elia Digha  akizungumza katika moja ya kikao  mkoani hapa hivi karibuni.

 

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: