WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini waongeze ubunifu wa kusukuma ajenda za Serikali kwa umma na si kusubiri kazi zifanywe na waandishi wa habari wengine.

“Mnapofanya kazi ongezeni ubunifu wa kusukuma ajenda za Serikali kwa umma na msisubiri kazi zifanywe na wanahabari wengine. Hakikisheni kila mwananchi anapata elimu na taaarifa sahihi kuhusu faida na umuhimu wa miradi na mipango au shughuli zinazotekelezwa na Serikali,” amesema.

Ametoa wito huo leo asubuhi (Jumatatu, Machi 27, 2023) wakati akifungua kikao kazi cha 18 cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini kilichoanza leo katika Kituo Cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu amesema: “Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini mnao wajibu wa kuhakikisha kuwa yale yote yanayopangwa na kutekelezwa na Serikali yanafahamika kwa umma wa Watanzania kwa usahihi, kwa wakati na kwa tija.”

Amesema wanapofanya mawasiliano hasa ya kimkakati, wahakikishe wanafahamu lengo la mawasiliano wanayotaka kufanya, faida na matarajio ya kutekeleza mawasiliano husika, nani mlengwa wa mawasiliano hayo pamoja na kuchagua njia sahihi za mawasiliano.

“Nimeona nisisitize hayo kwa kutambua kuwa mafanikio ya Serikali hayana budi kufahamika kwa wananchi wote na ni wajibu wa kila taasisi kuhakikisha mawasiliano hayo yanakuwa ya kimkakati ili yaweze kuleta tija na kufikia malengo yaliyokusudiwa.”

Ili kuwawezesha maafisa hao kutekeleza majukumu yao, Waziri Mkuu amewaagiza Makatibu Wakuu wote, Wakurugenzi wa Halmashauri na taasisi zote za umma watenge bajeti ya kutosha kugharamia shughuli za utoaji wa taarifa pamoja na elimu kwa umma na kuhakikisha jukumu hilo linatekelezwa kwa tija na ufanisi uliokusudiwa.

Pia amewataka viongozi wa wizara na wakuu wa taasisi waweke kipaumbele cha kuwashirikisha maafisa habari kwenye vikao mbalimbali ikiwemo vikao vya menejimenti ili waweze kwenda na wakati na kupata ufahamu wa kutosha wa taasisi na mipango ya Serikali.

Mapema, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari alisema wizara hiyo ipo katika hatua za mwisho kukamilisha utayarishaji wa Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano kwa Umma (The National Communications Strategy) ambao ukikamilika utaainisha na kufafanua utaratibu wa upatikanaji na usambazaji wa taarifa za Serikali kwa umma.

“Pamoja na mkakati huo, tuko kwenye hatua za mwisho za uandaaji wa Mkakati wa Mawasiliano Serikalini wakati wa Majanga (Risk Communication Strategy) na Mkakati wa Taifa wa Kujitangaza (National Branding Strategy).”

Pia alimkabidhi tuzo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua na kuthamini mchango wake katika kuimarisha sekta ya habari, demokrasia, uwazi, uhuru wa kutoa maoni na kupata taarifa nchini.

Share To:

Post A Comment: