Wananchi wa  wa vijiji vya Gaghata,Nyabat na Bassodesh kata ya Bassodesh wilayani Hanang', mkoa wa Manyara wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari wakati wakitoa malalamiko ya kuporwa mashamba yao mwishoni mwa wiki wilayani humo.

 Dotto Mwaibale na Thobias Mwanakatwe, Hanang.

WANANCHI wa vijiji vya Gaghata,Nyabat na Bassodesh kata ya Bassodesh, wilayani Hanang' mkoa wa Manyara wamemuomba Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuingilia kati wapate haki yao kutokana na kunyang'anywa maeneo ya mashamba yao zaidi ya  ekari 1500 na kusababisha wakose sehemu za kuendesha kilimo na ufugaji.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti ambao walifika katika vijiji hivyo, walisema maeneo hayo wamenyang'anywa na Hospitali ya Hydom (Hydom Lutheran Hospital) inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT).

Walisema wamelazimika kumuomba Rais Samia aingilie kati mgogoro huo ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 30 bila kupatiwa ufumbuzi ambapo viongozi wa wilaya wameshindwa kumaliza tatizo hilo ambalo limekuwa na sintofahamu nyingi na hivyo kusababisha wananchi kupata mateso.

Walisema katika hali ya kushangaza kila wanapokwenda kulalamikia haki yao katika ngazi nyingine za serikali baadhi ya viongozi wakiwamo wanasiasa wastaafu ambao wanatajwa kuhusika katika mgogoro huo wamekuwa wakitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ambao huenda kuwakamata na kuwaweka ndani wananchi wanaoonekana kuwa mstari wa mbele kufuatilia suala hilo.

Mmoja wa wananchi waliopata kadhia ya kukamatwa na polisi mwishoni mwa wiki iliyopita ni Qwari Sulle mkazi wa kijiji cha Bassodesh ambaye alikamatwa na polisi wa kituo cha Bassotu na baadaye kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Hanang' ambako alilala huko hadi siku ya pili alipoachiwa kwa kujidhamini mwenyewe na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) George Katabazi kuthibitisha tukio hilo.

Sulle ambaye eneo lake la ardhi ni  ekari 90  alilopewa na baba yake limechukuliwa na Hospitali ya Hydom, aliwekwa ndani kituo cha polisi kwa kile kilichoelezwa kuwa ni agizo kutoka kwa kigogo mmoja wa serikali wilayani kufuatilia kiongozi mmoja wa kisiasa mstaafu  kulalamika kuwa mwananchi huyo aliwapeleka wanahabari kijijini hapo.

Aidha, wananchi wa vijiji hivyo wamempongeza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Katabazi kwamba amekuwa msaada kwao kwani kila wanapokamatwa bila ya sababu za msingi taarifa zinapo mfikia amekuwa agiagiza kuachiwa.

Wananchi hao walisema wamekuwa wakifuatilia haki zao tangu mwaka 1990 ambapo Oktoba 15, 2012 waliandika barua katika ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya ya Hanang' kuomba wasaidiwe suala hilo lakini hadi sasa hakuna ufumbuzi wowote uliopatikana.

"Wamekuja wakuu wa wilaya kadhaa katika wilaya yetu akiwamo wa sasa  lakini kila wanapoelezwa jambo hilo wanapata ganzi kulishughulikia hali inayotupa mashaka makubwa kuna nini nyuma ya pazia katika suala hili," walisema.

Walisema kuna kipindi ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Hanang' iliandika barua yenye kumbukumbu namba HANDC/V.2/90/7 ikielekeza kusimamisha shughuli zote kwenye eneo la Waredick ambalo pia limechukuliwa na Hospitali ya Hydom lakini maelekezo yote yalipuuzwa.

Waliongeza kubwa mwaka 2016 waliandika barua kwenda kwa Kamishna wa Ardhi kanda ya Kaskazini kuomba utatuzi wa mgogoro huo lakini bado licha ya ufuatiliaji uliofanywa na ofisi ya kamishna ukipuuzwa.

Meneja wa Hospitali ya Hydom, Daniel Didaguy, alipoulizwa kuhusu malalamiko ya wananchi hao kwa njia ya simu alisema yupo kwenye gari hawezi kujibu lolote na kumuomba mwandishi asubiri atakapofika safari yake atampigia.

Hata hivyo, saa mbili baadaye alipopigiwa simu mara mbili hakupokea tena simu ilikuwa ikiita tu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Hanang', Janeth Mayanja , alipotafutwa  kwa kupigiwa simu ilikuwa ikiita na kukatwa  na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (SMS) hakujibu siku hiyo hadi baada ya siku mbili ambapo alikuja kujibu kwa kifupi kwamba, nanukuu " ila Hydom wamepewa muda mrefu mashamba hayo".

Hata hivyo, Mkuu huyo wa wilaya hakuweza kufafanua utaratibu uliotumika kuwapa Hospitali ya Hydom mashamba  hayo wala kueleza kwanini bado kuna malalamiko ya wananchi wa vijiji hivyo kama taratibu zilifuatwa wakati wa kuipa hospitali hiyo eneo linalolalamikiwa na wananchi.

Diwani mstaafu wa kata ya Bassodesh,Elisha Awwe , ambaye analalamikiwa na wananchi hao kuwa ndio chanzo cha mgogoro huo, alipofuatwa na mwandishi ili atoe ufafanuzi wa suala hilo alikataa kuzungumza na kuanza kumtupia lawama mwenyeji aliyeongozana na mwandishi huyo.

"Siwezi kuzungumza na mtu nisiyemjua,kama ungekuwa upo peke yako (mwenyeji) ningekusikiliza kwasababu nakufahamu," alisema diwani huyo mstaafu na kisha kufunga geti la mlango wake akidai anakwenda kusali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Bassodesh, Daniel Diaagwa,alipopigiwa simu kutaka afafanua mgogoro huo alisema yeye na wenzake ni viongozi wapya na kwamba wanaoufahamu vizuri mgogoro huo ni viongozi wastaafu akiwamo aliyekuwa diwani wa kata ya  Bassodesh.

Naye Diwani wa sasa wa Kata ya Bassodesh,Gawu Bajuta, alipopigiwa simu alijibu kuwa anaufahamu vizuri mgogoro huo na kwamba yupo ndani ya basi anasafiri akifika safari yake atatoa ushirikiano kwa kutoa maelezo kwa kina kuhusu mgogoro huo.

Hata hivyo, siku ya pili alipotafutwa diwani huyo kila alipopigiwa simu ilikuwa ikiita bila kupokelewa kwa mfululizo wa siku mbili.

Kufuatia malalamiko hayo, Mbunge wa Hanang' Mhandisi Samweli Xaday, alipopigiwa simu alikiri kuufahamu mgogoro huo na kuahidi Februari 17 mwaka huu (2023) ataenda katika vijiji hivyo kuitisha mkutano wa wananchi akiwa ameambatana na wataalamu wa ardhi wa wilaya.

Xaday alisema kamwe hatakuwa tayari kuona wananchi wake wanaonewa na kwamba ikiwezekana ataupeleka mgogoro huo kwenye vyombo vya sheria ukatafsiriwe.


Mzee Tlehhema Sulle baba mzazi wa Qwari aliyempatia mwanaye huyo shamba la ekari zaidi ya 90 ambalo alianza kuliendeleza tangu mwaka 1979 kabla na baadaye kuchukuliwa na hospitali hiyo ya Hydom inayomilikiwa na KKKT wakidai ni lao baada ya kufika katika kijiji hicho mwaka 1990.


Qwari Sulle (kulia) ambaye amekuwa akipata adha ya kukamatwa mara kwa mara na polisi wakati akifuatilia haki ya kupata shamba lake akiwa na familia yake na mama yake mzazi nje ya nyumba yake. Qwari hana hata sehemu ya kulima baada ya mashamba yake yote kuchukuliwa na kubakiwa na nyumba zake na hajui hatima ya maisha yake.

Muonekano wa mashamba yake yaliyochukuliwa na hospitali hiyo ambayo inadaiwa yamekodishwa kwa watu mbalimbali na kulimwa 
Ni baadhi ya magogo yaliyokatwa na hospitali hiyo na kuwekwa kuzunguka uzio wa boma la Qwari ikiwa ni njia ya kumuondoa katika eneo hilo.
Mashamba ya Qwari yaliyolimwa na hospitali hiyo baada ya kunyang'anywa.
Ni moja ya shamba ambalo likiwa lake ambalo amelima mahindi ili kujikimu na njaa lakini limesababisha kukamatwa na polisi kwa shinikizo la hospitali hiyo akidaiwa kuvamia shamba hilo na kulima.
Baadhi ya ng'ombe wa Qwari wakiwa katika boma, Ng'ombe hao wanakosa kwenda malishoni baada ya eneo lote la malisho kuchukuliwa na kanisa hilo.

Ni sehemu ya mbuzi na kondoo wa Qwari ambao kama hatua za makusudi hazitachukuliwa zitakosa malisho kutokana na mashamba yake kuchukuliwa na kanisa hilo. 
Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: