Mjumbe wa Halmashauri Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa(MNEC), Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula,ametaka wanafunzi 7,ambao bado hawajaripoti kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Igogwe watafutwe wao na wazazi wao.
Kwani imeelezwa kuwa kuna baadhi ya wanafunzi hao baada ya kumaliza darasa la saba walitoroka nyumbani huku wengine wakiwa wameolewa.
Dkt.Angeline ameeleza hayo wakati alipotembelea shule ya sekondari Igogwe Kata ya Bugogwa kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa miradi ya kupunguza umaskini(TPRP IV-OPEC) ikiwemo ujenzi wa bweni la wasichana 80 katika shule hiyo,ikiwa ni sehemu moja wapo ya ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo jimboni Ilemela, iliofanyika Februari 18, mwaka huu.
Ameeleza kuwa katika shule hiyo, ilipangiwa wanafunzi 167,wa kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo wa 2023 kati yao 160 wameripoti shuleni hapo huku 7 wakiwa hawajaripoti na sababu zikielezwa kuwa baadhi yao wameolewa na wengine walitoroka nyumbani.
Hivyo hawawezi kusema kwamba hatua wameisha chukua,jarada limeisha andikwa na Polisi bado hawajawapeleka mahakamani,wanafanya mchezo wa kuigiza ambapo aliomba jambo hilo lisimamiwe na wanahusika washughulikiwe.
“Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya hao watoto saba na wazazi wao lazima wapatikane kama kushitakiwa anashitakiwa mzazi na mtoto,haiwezekani Rais anatoa fedha ya kutosha ya kuweka miundombinu,milioni 516 kwa Kata moja,shule moja siyo haba lakini wao hawatipoti shule,”ameeleza Dkt.Angeline.
Pia ameeleza kuwa,wanataka watoto wote waendelee na shule hawataki kuona mtoto anaishia darasa la saba ingizingatiwa shule wamesogezewa karibu ambapo awali walikuwa wanakimbia mimba matokeo yake sasa watu wanaozesha.
Huku akihoji kuwa hivi mzazi wa namna hiyo wanamchukuliaje,jambo hilo ameisha likabidhi kwa Mkuu wa Wilaya na la msingi hatua zichukuliwe.
“Kwenye elimu hatutaki mchezo tunachohitaji watoto wote wasome,niwapongeze kuwa ni kiwago kidogo cha wanafunzi ambao hawajaripoti lakini taarifa zao siyo nzuri kwa sababu wengine wameolewa,wengine wamekimbia hapana lazima wapatikane na bahati nzuri Rais aliisha ridhia mtoto akipata ujauzito anapata fursa ya kuendelea na masomo watafutwe waendelee na shule,”ameeleza Dkt.Angeline.
Awali akizungumza mbele ya Mbunge huyo,Mkuu wa shule ya sekondari Igogwe Atanas Manyika, ameeleza kuwa shule hiyo kwa mwaka mpya wa masomo 2023, shule hiyo ilipangiwa wanafunzi 167 wa kidato cha kwanza lakini mpaka sasa wameripoti wanafunzi 160.
“Hatuna taarifa rasmi sana lakini zilizopo zinasemekana kuwa wengine wameolewa na wengine walitoroka baada ya kumaliza darasa la saba,taarifa tumeisha zipeleka ngazi ya Kata ambao watazifuatilia na kuchukua hatua zinazofaa kwa mujibu wa sheria,”ameeleza Mwl.Manyika.
Ikumbukwe kuwa mwaka 2022, Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango,akiwa mkoani Mwanza katika ziara ya kikazi akizungumza mara baada ya kuzindua mradi wa stendi ya kisasa ya mabasi na maegesho ya malori ya Nyamh’ongolo wilayani Ilemela,alikemea mimba na ndoa za utotoni kwani ni kinyume na sheria na inachangia watoto kutofikia malengo na ndoto zao.
Hivyo aliwaagiza viongozi wa Mkoa wa Mwanza kuhakikisha watoto wanasoma na wasisite kuchukua hatua za kisheria kwa wale watakaokiuka na kuhusika kwa namna yoyote kukatisha masomo kwa mtoto wa kike .
Aidha Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha kuwa mtoto wa kike anatimiza ndoto zake za kielimu na akatishi masomo.
Ambapo katika bajeti ya mwaka 2022/2023 kwa upande wa elimu serikali ilifuta ada ya kidato cha tano na sita, hivyo kufanya elimu kuanzia ngazi ya elimu ya msingi mpaka kidato cha sita kuwa ni bila malipo sanjari na kuhakikisha imejenga madarasa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza pamoja na kupiga marufuku baadhi ya michango ambayo ingekwamisha mtoto kujiunga na kidato cha kwanza ambapo Halmashauri ya Ilemela ilipokea kiasi cha bilioni 2.2 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 110 kwa shule za sekondari 23,zilizokiwa na upungufu wa madarasa hayo na kufikia Desemba 21, ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa ulikuwa umekamilika.
Post A Comment: