Mbunge wa viti maalum kupitia chama cha mapinduzi CCM Mkoa wa Iringa Nancy Nyalusi akiongea na viongozi mbalimbali baada ya kuwasili kwenye Kijiji cha Ilalasimba ambako kunajengwa wodi ya wanawake aliyochangia Milioni 10.
Mbunge wa viti maalum kupitia chama cha mapinduzi CCM Mkoa wa Iringa Nancy Nyalusi akiteta Jambo na Diwani wa kata hiyo Stephen Mhapa na katibu wa chama cha mapinduzi wilaya ya Iringa Gama Gama wakati wa mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Ilalasimba.

Na Fredy Mgunda, Iringa.


MBUNGE wa Viti Maalum kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa Nancy Nyalusi ametoa Shilingi Milioni 10 kuchangia ujenzi wa wodi ya wanawake katika zahanati ya Kijiji cha Ilalasimba kata ya Nzihi kwa lengo la kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Ilalasimba,Mbunge Nancy Nyalusi alisema kuwa kujengwa kwa wodi hilo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya mama na mtoto ambavyo vimekuwa vikitokea Mara kwa Mara.

Nyalusi alisema kuwa ametoa kiasi cha shilingi millioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ikiwa ni kutimiza wajibu wake kwa jamii kama ambavyo Ilani ya chama cha mapinduzi CCM ya mwaka 2020/2025 inavyotaka wabunge kuwatumikia wananchi.

Alisema kuwa bado kunachangamoto nyingi katika Kijiji hicho hivyo ataendelea kushirikiana na uongozi wa Kijiji na kata kutatua changamoto hizo kwa kuwa yeye ni Mbunge wa mkoa wa Iringa.

Mbunge Nyalusi alisema kuwa diwani wa kata hiyo Stephen Mhapa ndio aliyemueleza changamoto ya ujenzi wa wodi hiyo hivyo aliamua kumuunga mkono kwa kutoa kiasi hicho cha fedha na ataendelea kuchangia kila Mara kwenye shughuli za kimaendeleo.

"Mimi kwa nafasi yangu kama Mbunge nina wajibu wa kuona njia ya kusaidia kutatua kero zenu wananchi na ndio maana leo nipo hapa, na kwa kuwa nina guswa na kero ya afya leo nimeleta kiasi cha Shilingi Milioni 10 ili zisaidie kujenga wodi ya wanawake kwenye zahanati hii ya kijiji chenu"alisema Nyalusi

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Nzihi ambaye ni mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa Stephen Mhapa alisema kuwa anampongeza Mbunge Nancy Nyalusi kwa kujitolea kusaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto kwa kuchangia ujenzi wa wodi ya wanawake.
Share To:

mwangaza wa hbari

Post A Comment: