Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula

********************************

Na Munir Shemweta, WANMM

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 90.9 katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Disemba 2022 kama kodi ya pango la ardhi sawa na asilimia 75 ya lengo la makusanyo ya shilingi bilioni 121.

Aidha, makusanyo ya mwaka wa fedha 2022/2023 yameongezeka kwa shilingi bilioni 33.9 ikilinganishwa na kipindi kama hiki kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Kuongezeka kwa makusanyo kumechangiwa na msamaha wa riba ya malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi ambapo wananchi walio na malimbikizo walipewa nafuu ya kulipa deni la msingi kuanzia julai hadi desemba 2022 uliotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Hayo yalibainishwa leo tarehe 7 Februari 2023 na Waziri wa Ardhi Nyumba an Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ulipaji kodi ya pango la ardhi na maduhuli mengine ya sekta ya ardhi mkoani Dodoma.

Hata hivyo, Dkt Mabula alisema, Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kuongeza kipindi cha msamaha hadi April 2023 na kubainisha kuwa, uamuzi huo ulifikiwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo maombi mengi ya wananchi na taasisi yaliyoifikia serikali.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, wananchi 6,211 wameufaika na msamaha wa riba ya malimbikizo sawa na shilingi 11,931,537,409.80.

‘’Serikali inaamini kuwa fedha zilizosamehewa zimeenda kuleta nafuu kwa wahusika na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii nchini na nimshukuru Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kuwasamehe kisi kikubwa hicho cha pesa kwa lengo la kuwaondolea mzigo wananchi na taasissi mbalimbali’. Alisema Dkt Mabula.

Ametoa rai kwa taasisi na mashirika ya umma na wananchi wote kutumia muda uliotolewa hadi April 30, 2023 kunufaika na msamaha wa riba uliotolewa na serikali kulipa deni la msingi (Principa amount) ili wasamehewe riba ya malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi.

Ameelekeza ofisi zote za ardhi nchini kutoa huduma siku zote hadi mwisho wa mwezi April 2023 ili kuwezesha upatikanaji huduma za ukadiriaji kodi kwa wakati na kuwasihi wananchi kuendelea kutumia njia za kielektroniki alizozieleza kuwa zimeanza kutolewa na benki washirika za CRDB na NMB katika kukadiria kulipa kodi.

‘’Waandishi wa habari wajulisheni wananchi kuwa Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameongeza muda wa msamaha wa riba ya malimbikizo na Wizara imejipanga kikamilifu ili kuwezesha wananchi kupata nafuu ya msamaha wa riba ya kodi ya pango la ardhi iliyotolewa’’ alisema Dkt Mabula.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: