Na Elizabeth Joseph,Arusha.


Vijiji zaidi ya 50 vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara vimenufaika na hifadhi hiyo kwa kupatiwa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Barabara,Maji na Madarasa.Hayo yamesemwa na Mhifadhi Daraja la kwanza kitengo cha Utalii Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara Bw,Ahmed Nassoro wakati akiongea na Wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha walipotembelea Hifadhi hiyo.


Nassoro alisema kuwa ili kuimarisha mahusiano mazuri baina ya Hifadhi na Jamii inayozunguka Hifadhi hiyo miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Vyumba vya Madarasa,Bweni,nyumba za Waganga wa Afya pamoja na vituo Vya afya imekuwa ikitekelezwa katika vijiji hivyo ili kusaidia wananchi.


Mbali na hilo aliongeza kuwa elimu ya uhifadhi imekuwa ikitolewa kwa wakazi wa Vijiji hivyo ikiwa ni pamoja na ziara za mafunzo hifadhini ili kulinda na kuendeleza shughuli zote uhifadhi na hivyo kuendeleza Utalii nchini.


Aidha alibainisha kuwa ili kusaidia wakazi hao kujiinua kiuchumi Hifadhi hiyo pia imesaidia katika miradi ya ufugaji nyuki pamoja ujasiriamali mbalimbali na kutengeneza mipango bora ya ardhi jambo alilosema limesaidia wengi kujiendeleza kimaisha.


Kuhusu hali ya Utalii hifadhini hapo Nassoro alipongeza jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania MH,Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutangaza vivutio vinavyopatikana Tanzania na kusema jambo hilo limeongeza kasi ya wageni kutoka Nchi mbalimbali kufika hifadhini hapo.


Nassoro pia aliwataka watanzania kujivunia vivutio vilivyopo kwa kutembelea ili kufanya shughuli za Utalii pamoja na kutangaza Utalii unaopatikana nchini ili kuhamasisha wageni wa Nchi tofauti kufika Tanzania na kuona vivutio hivyo.


Naye mmoja wa Waandishi wa Habari Mwanaidi Bundala aliishukuru Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa kwa kuamua kutembelea Hifadhi hiyo na kusema inawakumbusha kuzidi kutangaza Utalii nchini ili kuinua Uchumi wa Tanzania kupitia wageni kutembelea vivutio.


Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara ni moja kati ya Hifadhi maarufu yenye sifa ya kuwa na Simba wanaopanda miti,Hifadhi inayozungukwa na ukuta wa Bonde la ufa pamoja na kuwa makundi ya wanyama ya Tembo,Nyati na wanyama wengine pamoja na sehemu ya maji Moto yenye nyuzi joto 60 hadi 70.

Share To:

Post A Comment: