Na Elizabeth Joseph, Monduli.


VIJANA wilayani Monduli Mkoa wa Arusha wameshauriwa kujitambua katika kufanya maamuzi na kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi ili kuwa na taifa lenye afya bora baadaye.

Ushauri huo umetolewa Disemba 3 na Katibu Tawala Wilaya ya Monduli Robert Siyantemi akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo Mh,Frank Mwaisumbe wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani ambayo kwa Wilaya ya Monduli yameadhimishwa siku hiyo huku yakiwa na Kauli mbiu ya Haki na Usawa.


Siyantemi alisema kuwa ili kujenga taifa imara na wachapakazi ni muhimu vijana hao kutambua na kutimiza malengo yao kielimu,afya na hata katika maisha yao ya kila siku ikiwa ni pamoja na kuepuka vishawishi vyote vinavyoweza kuwasababishia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.


"VIJANA jukumu lenu ni kuleta mabadiliko ya kiuchumi, maendeleo na mengine mengi mazuri katika taifa letu na juhudi hizi zinaweza zisifanikiwe kutokana na janga hili la Ukimwi hivyo lazima mjitambue nyie ni nani na mtambue umuhimu wenu katika taifa letu kwa baadaye"aliongeza kusema.

Kwa upande wake Mratibu wa kudhibiti Ukimwi upande wa Utabibu Wilaya ya Monduli Dkt,Winnie Letee alibainisha lengo la kongamano hilo kuwa ni wenye umri wa miaka 15 hadi 30 ambao wako katika hatari ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Aidha alieleza kuwa kwa Kipindi Cha miaka mitatu idadi ya maambukizi kwa kundi hilo la vijana imekuwa ikiongezeka tofauti na makundi mengine ambao wao idadi ya maambukizi imekuwa ikishuka.


"Mwaka 2019/20 maambukizi ilikuwa ni asilimia 2.8 huku mwaka 2021/22 maambukizi ilikuwa ni asilimia 3.2"alibainisha Dkt Winnie.


Naye Mwenyekiti wa Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi wilayani Monduli Bw, Abdallah Hamis aliwataka wanaoishi na Virusi vya Ukimwi kuzingatia masharti wanayopewa ikiwemo kuhakikisha wanameza dawa za kufubaza makali ya VVU.


"Kufa mapema wewe mwenyewe utakuwa umetaka kwa kutozingatia masharti ya umezaji dawa,na kwa wale waliogundulika kuwa na maambukizi wasisite kujitokeza na kuanza kliniki ya matunzo na tiba ili waweze kuishi maisha marefu na kuwa na furaha kama wanavyoishi wengine kwakuwa Virusi vya Ukimwi haviui ukifuata masharti yake"aliongeza kusema Bw,Hamis.


Kongamano la maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani wilayani Monduli lilihusisha wanafunzi wa Chuo Cha Maendeleo ya Jamii pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Irkisongo na Engutoto zilizopo wilayani humo.

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: