Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Mkoa wa Singida, Shukrani Mbago akizungumza  katika mafunzo ya kuwajenge uwezo watu wenye ulemavu kutoa taarifa pale wanapofanyiwa ukatili, mafunzo  yaliyoendeshwa na ESTL leo Desemba 7, 2022 mjini hapa.

Na Dotto Mwaibale, Singida 

SHIRIKA la Empower Society Transform Lives (ESTL) linalojihusisha na masuala ya kupinga ukatili wa kijinsia katika muktadha wa dhana hasi ya kuondokana na vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto kwa  ufadhili wa Shirika la Foundation Civil Society (FCS)  limetoa mafunzo ya kuwajenge uwezo watu wenye ulemavu ili waweze kutoa taarifa pale wanapofanyiwa ukatili.

Mafunzo mengine yaliyotolewa ni pamoja dhana ya ujinsia na ukatili wa kijinsia na aina nyingine za ukatili wa kijinsia zinazoripotiwa katika kata,vijiji,mitaa,sheria na mikataba mbalimbali ya kimataifa kuhusu dhana ya ukatili wa kijinsia na ukeketaji. 

Pia mafunzo mengine yaliyotolewa ni fursa za kijasiriamali toka halmashauri, miongozo ya upatikanaji wa mikopo,mfumo wa upatikanaji wa mkopo wa halmashauri hasa asilimia mbili ya fedha za mkopo inayotolewa kwa kundi la watu wenye ulemavu mafunzo yaliyotolewa na Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Mkoa wa Singida, Shukrani Mbago. 

Katika mafunzo hayo Mbago alitoa wito kwa jamii hasa wazazi kuhakikisha  wanawalinda watoto wao dhidi ya ukatili kwa kuripoti vitendo vya ukatili sehemu husika ili wanaotenda vitendo hivyo waweze kuchukuliwa hatua. 

Afisa Mawasiliano na Vijana wa ESTL, Edna Mtui alitoa mafunzo yaliohusu dhana ya mila potofu na ndoa za utotoni, ndoa za kulazimishwa, na athari zake, dhana ya ukeketaji na athari zake na usafirishaji haramu wa binadamu. 

Mtui alisema kwa sasa kuna vitendo vingi vya ukatili wa kijinsia katika jamii ambao upo wa aina tano ukiwepo ukatili wa kiuchumi ambao wakina mama wanaupitia hasa  pale baba anapouza  mazao yote licha ya mama kushiriki katika uzalishaji.

Aidha Mtui aliongeza kuwa kuna vipigo ambavyo akina mama wengi wanavipata majumbani na ukatili wa watoto wengi kuachishwa masomo yao ili waweze kuolewa.

Alisema kuna watu wengine wapo wanafanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia pasipo wao kujua, hivyo elimu ni muhimu kwa jamii ili iweze kutambua vitendo vyote vya ukatili.

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Kutokomeza Ukeketaji na Ukatili wa Kijinsia  wa ESTL  John Nzungu alisema bado kuna baadhi ya wazazi wanawaficha watoto wenye ulemavu na kuwakosesha haki yao ya msingi ya kupelekwa shule.

Nzungu aliongeza kuwa mila na desturi pia bado ni changamoto ambapo watoto wenye ulemavu hawapelekwi kliniki wakiona ni aibu kuwa na mtoto mwenye ulemavu, sababu hiyo inasababisha kushindwa kupata huduma za afya.

 Mwenyekiti wa Watu wenye Ulemavu Mkoa wa Singida, Boniphace Kitiku alisema ukatili kwa watu wenye ulemavu ni mkubwa  licha ya kuwepo wadau wengi wanaoshughulika  kutoa elimu ya usawa kwa watu wote ili watu wa kundi hilo wasifanyiwe ukatili.

Kitiku alitoa wito kwa jamii kuwaona walemavu nao ni watu ambao wanaweza kuishi pamoja kama Mungu alivyowajaalia lakini bado kuna mitazamo hasi kutoka kwa baadhi ya watu wakiona walemavu ni mtaji wa kukuza biashara hasa zile kubwa na kuwatafutia balaa baada ya kudanganywa na waganga wa kienyeji.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameiomba serikali na wadau mbalimbali kuendelea  kutoa elimu ya kupambana na ukatili wa kijinsia ili kupunguza vitendo hivyo ambavyo bado baadhi ya watu wanaendelea kuvifanya.

Wamesema kuwa baadhi ya wazazi bado wanashikilia mila na desturi zilizopitwa na wakati ambazo zinasababisha vitendo hivi kuendelea kufanyika ikiwa ni pamoja na kusema binti kufanyiwa ukeketaji ni kutolewa mikosi.

Wameongeza kueleza kuwa  imani za kishirikina zinachangia kuwepo kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kutafuta  utajiri, hali inayosababisha ubakaji kwa watoto, wazee, wagonjwa wa akili kwa dhana kuwa wakitaka kufanikiwa ni lazima wafanye hivyo kama wanavyoambiwa na waganga wa kienyeji.

Mratibu wa Mradi wa Kutokomeza Ukeketaji na Ukatili wa Kijinsia kutoka Shirika la ESTL John Nzungu (kulia) akizungumza.
Afisa Mawasiliano na Vijana wa shirika hilo Edna Mtui (kushoto) akitoa mada kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.

Mwenyekiti wa Watu wenye ulemavu Mkoa wa Singida, Boniphace Kitiku, akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Afisa Mawasiliano na Vijana wa shirika hilo Edna Mtui (kulia) akiteta jambo na Ofisa wa shirika hilo, Aisha Msuya.

Picha ya pamoja baada ya mafunzo hayo.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: