SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Tulia Ackson pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM Tanzania Bara Abdulurhaman Kinana wameelezea kuhusu kasi ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa Bwawa la kufua umeme megewati 2115 huku wakitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya ya kuwatumikia Watanzania na kutekeleza miradi ya kimkakati nchini.

Akizungumza mbele ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan wakati wa tukio la kuanza kujaza maji kwenye bwawa la Julius Nyerere baada ya ujenzi wake kufikia asilimia 78, Spika wa Bunge Dk.Tulia amesema tukio la leo Desemba 22, 2022 linatengeneza historia ya kuondoa tatizo la umeme nchini kwa maana ya kutafuta suluhu ya kudumu. 

“Rais Dk.Samia Suluhu Hassan umefanya,unafanya na kuzidi.Salamu yako inayosema nawasilimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tunaitikia Kazi iendelee ni kweli tunashuhudia kazi inaendelea.

“Leo tuko hapa na baadhi yetu yetu tumetembelea mradi, inapotajwa kwamba tumefikia asilimia 78 ya mradi ule ni wastani wa jumla tu.Tumepita maeneo mbalimbali ya mradi huu kuna maeneo ujenzi umefikia asilimia 97, maeneo yamefikia asilimia  87 na mengine asilimia 80 na kuzidi.

 “Mradi huu mbali ya kuzalisha umeme pia unagusa maeneo mengine yakiwemo ya upatikanaji wa maji kwa Mkoa wa Dar es Salaam , Pwani na mikoa mingine. Tunatamani Ilani ya uchaguzi Mkuu inaposema umeme ufike vijiji vyote na maji yapatikane kwa asilimia 85 vjijini na asilimia 95 kwa miji, kupitia bwawa hili tunaamini tunakwenda kufikia asilimia hizo.”

Ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa Bunge litasaidia kukamilika kwa mradi huo na kwamba watakwenda kuwaambia wananchi kuwa Rais Dk.Samia amefanya, anafanya na kuzidi.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Kanali mstaafu Abdulurhaman Kinana amesema  mradi huo ni sehemu ya utekekelezaji wa Ilani ya CCM iliyotolewa kwa Watanzania.

“Watanzania wanaamini baada ya kukamilika kwa bwawa hili umeme utasambazwa katika kwa wingi kwenye maeneo mbalimbali ya nchi yetu na utakuwa wa bei nafuu. Napongeza kasi ya ujenzi wa mradi huu.Nikuahidi mimi na wenzangu tutafanya ziara ya kutembelea mradi huu ili tuufahamu lakini kuwapa moyo watendaji wake.”

Share To:

Post A Comment: