HALMASHAURI Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi imeliengua jina la Mbunge wa Jimbo la Kisesa wilayani Meatu Mkoa wa Simiyu, Luhaga Mpina kwenye kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM (NEC) Mkoa wa Simiyu.

Katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mohamed Ali Khalfan amesema jina la Mpina halimo kwenye orodha ya majina matatu ya wagombea wa nafasi ya NEC Mkoa wa Simiyu yaliyopitishwa na vikao vya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.

Mpina alikuwa ni miongoni mwa makada wa CCM waliochukua na kurejesha fomu kuomba nafasi ya MNEC Mkoa wa Simiyu na NEC Viti 15 Tanzania Bara.

Hata hivyo Katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu , Khalfan amesema majina hayo ya walioteuliwa atayataja baadae kwani alikuwa kwenye uchaguzi wa Mwenyekiti wa UWT Mkoa.

Baadhi ya makada wa CCM wamedai kuwa huenda ikawa jina la Mpina limeenguliwa na vikao vya juu kutokana na misimamo yake anayoionyesha bungeni kuhoji mambo mbalimbali ambayo yanayowagusa wananchi.

Wamesema miongoni mwa mambo wanayohisi huenda yamemponza Mpina ni pamoja na kuhoji bungeni kuhusu madai ya fedha za makinikia Trilioni 360 akitaka kujua nani alisamehe na kama ana mamlaka kisheria kusamehe madai halali ya watanzania ya kiasi cha shilingi Trilioni 5.5 kama ilivyoamuliwa na Mahakama za rufani za Kodi za TRAB na TRAT.

Lingine ni kuhoji bungeni juu ya Serikali kushindwa kudai madai halali ya shilingi Trilioni 1.5 kwa ucheleweshaji wa mradi na CSR kutoka kwa Kampuni ya Arab Contractors ya Misri inayojenga mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Julius Nyerere. Lakini pia Serikali kuendelea kutoa taarifa zinazokinzana juu ya ukamilishaji wa mradi huo.

Mpina pia kupitia Bunge alihoji kuhusu kupaa kwa Deni la Taifa kutoka wastani wa kukua kwa asilimia 4 hadi asilimia 13 na kutojulikana zilipo shilingi Trilioni 5 zilizokopwa nje ya bajeti kwa mwaka 2022.

Mbali na hilo Mpina pia alihoji bungeni kitendo cha TRA kushindwa kukusanya malimbikizo ya kodi yasiyo na kesi mahakamani kiasi cha shilingi Trilioni 7.5 na ucheleweshaji wa maamuzi ya mapingamizi ya kodi katika mahakama za rufani za kodi kiasi cha shilingi Trilioni 5 bila kuwepo sababu za msingi.

“Kuhoji kwake bungeni uhalali wa malipo yaliyofanywa na Serikali kwa Kampuni ya Symbion LLC ya shilingi Bilioni 350 nje ya bajeti na bila kuzingatia madai halali ya Serikali ikiwemo kodi na gharama nyinginezo huenda nalo limemgharimu” amesema Jumanne Mashauri Mkazi wa Bariadi.

Jambo lingine linalodaiwa kumponza Mpina ni kukataa bungeni juu ya uamuzi wa Serikali kujenga Bandari ya Bagamoyo bila kuwepo tathmini ya kina juu ya uwezo wa kiuchumi kugharamia mradi huo.

Suala lingine linalodaiwa kumponza Mpina ni kitendo chake cha kuhoji bungeni kuhusu Serikali kuingia mikataba mibovu, kushindwa kurejesha ng'ombe 6,000 za wafugaji walioshinda kesi mahakamani, Serikali kushindwa kudhibiti tembo wanaovamia mashamba na makazi ya wananchi na kusababisha vifo na majeruhi.

Jambo lingine ni kuhoji bungeni kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta kwa kisingizio cha vita ya Urusi na Ukraine hali iliyoilazimu Serikali kuweka ruzuku ya shilingi bilioni 100 kila mwezi bila kuwepo unafuu wowote kwa wananchi.

Hata hivyo wananchi hao wamesema huenda pia msimamo wake wa kuhoji bungeni suala la katakata ya umeme na migao ya umeme isiyoisha nchini iliyopelekea kuathiri uchumi na utoaji wa huduma zinazotegemea nishati ya umeme huenda pia likawa limemgharimu kuenguliwa.

Maeneo mengine ambayo Mpina amekuwa akihoji bungeni ni kuhusu suala la usimamizi mbovu na kupanda kiholela kwa bei ya mbolea na namna ilivyowaathiri uzalishaji na upatikanaji wa chakula nchini

Pia amekuwa akihoji bungeni juu ya kupanda kiholela kwa bei za bidhaa na gharama za maisha hali iliyopelekea mfumko mkubwa wa bei nchini huku Serikali ikishindwa kudhibiti hali hiyo.

Mpina alipoulizwa kuhusiana na madai ya kuenguliwa kwenye kinyang’anyiro cha NEC Mkoa wa Simiyu simu yake iliita bila kupokelewa na baadaye alituma ujumbe mfupi wa maandishi kuwa yuko kwenye kikao cha Kamati ya Fedha cha Halmashauri ya Meatu

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: