Naibu Waziri wa Kilimo, Mh. Anthony Mavunde aeleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali yenye lengo la kuhakikisha asilimia 60 ya korosho zote zinazozalishwa nchini zinabanguliwa ifikapo msimu wa mwaka 2025/2026.


Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo leo tarehe 31 Novemba, 2022 akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipokuwa akishuhudia mzigo tani 7.5 wa korosho zilizobanguliwa ukisafirishwa kwenda nchini Marekani na kampuni ya Ward Holding Tanzania (WHT).

"Leo tunashuhudia tukio la kihistoria, ambapo korosho iliyobanguliwa nchini Tanzania inaenda kuuzwa kwa mtumiaji wa mwisho nchini Marekani. Hii ni habari njema kwa wakulima wa korosho nchini na ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na Rais wetu mpendwa Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kufungua nchi kimataifa, hali inayopelekea kuongeza uhakika wa masoko ya mazao ya wakulima wetu.

Bei ya korosho ghafi nchini ni kati ya 1,800 hadi 2,200 ambapo unahitaji kilo tano za korosho ghafi ili kupata kilo moja ya korosho iliyobanguliwa. Wakati huo huo, bei ya korosho iliyobanguliwa nchini Marekani ni Dola za Kimarekani 40 (sawa na zaidi ya shilingi 90,000 za Kitanzania), hesabu hii inaonesha dhahiri kuwa kuuza korosho iliyobanguliwa kuna manufaa makubwa kwa wakulima wetu na Taifa kwa ujumla.

Wizara ya Kilimo inatekeleza mpango wake wa Ajenda 10/30 wenye lengo la kuhakikisha kilimo kinakua kwa wastani wa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, msukumo mkubwa kufikia lengo hilo upo katika upatikanaji wa masoko ya uhakika ambayo yatamvutia mkulima kulima kwa tija na faida.

Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Chama cha Wabanguaji Korosho Tanzania ili kuhakikisha tunakuza tasnia ya Korosho kwa kuongeza thamani hali itakayosaidia kuongeza kipato kwa wakulima na kuongeza mchango wa zao la korosho katika kukuza uchumi wa Taifa.

Nimefurahishwa kwa namna bidhaa hiyo ilivyoandaliwa na kuwekwa tayari kwa soko la Marekani na Watanzania wenyewe. "Kila kitu katika bidhaa hii, kuanzia kuibangua na kuiweka kwenye vifungashio vinavyovutia imefanywa hapa hapa Tanzania, hakika Watanzania tunaweza. Nitoe rai kwa Taasisi za fedha kuendelea kuunga mkono juhudi za wajasiriamali na sekta binafsi kwa ujumla ili iendelee kukua na kuwa na mchango chanya kama huu kwenye maendeleo ya sekta ya kilimo na nchi kwa ujumla"Alisema Mavunde

Naye Rais wa Kampuni ya Ward Holding Tanzania, Ndg. Godfrey Simbeye alieleza kuwa mahitaji ya korosho iliyobanguliwa nchini Marekani ni karibu mara 4 ya korosho tunayozalisha nchini kwa sasa, hivyo fursa ya soko ni kubwa, lenye faida zaidi kwa mkulima na Taifa kwa ujumla ukilinganisha na uuzaji wa korosho ghafi.

Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania,Mh. Robert Raines ameihakikishia nchi ya Tanzania katika ushirikiano wa kutosha ili kuwawezesha wakulima wa korosho kupata soko la uhakika nchini Marekani.






Share To:

Post A Comment: