KIJANA Piniston Nzali (20) mkulima anayeishi Kidete mkoani Morogoro amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka matatu ya kuchapisha mtandaoni taarifa yenye kuharibu hadhi ya Rais Samia Suluhu Hassan na Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete.

Mshtakiwa Piniston pia anashtakiwa kwa kosa la kushindwa kusajili laini ya simu iliyokuwa ikimilikiwa na mtu mwingine.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa serikali Sylivia mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Luboroga imedaiwa, Oktoba 8, 2022 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mshtakiwa alichapisha taarifa yenye kuharibu heshima au hadhi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Katika taarifa hiyo inadaiwa, mshtakiwa kupitia mtandao wa Tiktok alichapisha video inayomuonesha Rais Samia akiimba jambo ambalo halikuwa la kweli.

Mshtakiwa pia anadaiwa kuchapisha taarifa inayofanana na hiyo ikimuonesha Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete akiimba kosa alilolitenda Oktoba 10, 2022 huku akijua kuwa jambo hali siyo la kweli.

Aidha katika shtaka la mwisho, inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Oktoba 1, 2022 na Oktoba 20, 2022 mshtakiwa alitumia laini ya simu ambayo awali ilikuwa inamilikiwa na Benjamani Chaji bila kutoa taarifa ya mabadiliko ya umiliki kwa mtoa huduma.

Mshtakiwa amekana mashtaka hayo na amerudishwa mahabusu mpaka kesho kesi hiyo itakapotajwa atajwa kwa ajili ya kueleza hatua upelelezi ulipofikia
Share To:

Post A Comment: