Muonekano wa jengo la Kituo cha Afya cha Kata ya Ntuntu kilichopo wilayani Ikungi mkoani Singida ambacho kimetakiwa kuanza kutoa huduma za utabibu mara moja ifikapo Novemba, 28, 2022 baada ya ujenzi wake kukamilika kwa asilimia 99.
Wajumbe wa kamati ya ujenzi wa kituo hicho wakifanya ukaguzi wakiongozwa na Mkurugenzi wa Huduma za Afya Lishe na Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR- TAMISEMI) Dkt.Ntuli Kapologwe wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutembelea kituo hicho na kukikagua aliyoifanya wilayani humo hivi karibuni.
Ukaguzi wa kituo hicho ukifanyika.
Picha ya pamoja baada ya kukaguliwa kwa kituo hicho.

Na Dotto Mwaibale, Singida

WANANCHI wa  Kata ya Ntuntu Walayani Ikungi mkoani hapa wanatarajia kuanza kupata huduma za kitabibu katika Kituo kipya Cha Afya Cha  Ntuntu baada ya ujenzi wake kukamilika kwa asilimia 99.

Akizungumza  hivi karibuni wakati wa ziara yake Mkurugenzi wa Huduma za Afya Lishe na Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR- TAMISEMI) Dkt.Ntuli Kapologwe  amesema ifikapo jumatatu ya Novemba 28 mwaka huu kituo hicho kiwe kimeanza kazi na kuhudumia wananchi.

Aidha ameeleza kwamba  hatua iliyofikia kituo hicho  inastahili kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wa maeneo hayo wakati vitu vidogo vidogo vilivyobaki vikiendelea kukamilishwa.

Hata Hivyo Dkt.Kapologwe ameagiza Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa kushirikiana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida kuendelea na maandalizi ya kupokea vifaa tiba ili ifikapoa Novemba 28,2022 huduma ziwe zimeanza na wananchi wanapata matibabu.

"Tumeambiwa jengo limefikia asilimia 99 kukamilika kwa hatua hii ni lazima huduma zianze  kutolewa hata kama kuna vitu vichache vya kumalizia " alisema.

Hata hivyo ameendelea kueleza kwamba Serikali ipo hatua ya mwisho ya kuleta vifaa tiba katika kituo hicho ambapo amesema kufikia jumatatu vitakuwa vimeshafika.

"Serikali ipo kwenye hatua za mwisho za uletaji wa vifaa tiba mbalimbali katika kituo cha afya hivyo wananchi waanze kupata huduma"  alisema Dkt. Kapologwe.

Dkt. Kapologwe  ameipongeza  Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi na timu nzima ya usimamizi wa ujenzi wa kituo hicho cha afya kwa ukamilishaji mzuri wa majengo matatu ya awamu ya kwanza (Jengo la Wagonjwa wa Nje OPD, Jengo la Maabara na Kichomea Taka) ambao mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 99% .

Aidha  majengo  matatu mengine  ni pamoja na  Jengo la Wodi ya Wazazi (Maternity), Jengo la Upasuaji (Theatre) na Jengo la Kufulia (Laundry)  ambapo ujenzi huyo umefikia zaidi ya asilimia 60%  huku Dkt.Kapolongwe akiwataka kuongeza kasi ya ujenzi ili  kufikia Disemba 30 majengo hayo yawe yamekamilika.

Ujenzi wa vituo vya afya ni moja ya mkakati na kipaumbele cha serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia  kuhakikisha  wananchi wanapata huduma za afya katika maeneo ya karibu na makazi yako.

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: