Na Gift Mongi Moshi


Upendo amani na ushirikiano ni miongoni mwa nyenzo walizobebeshwa viongozi wapya wa chama Cha mapinduzi (CCM)ambao pia ni wajumbe wa halmashauri kuu kata ya old Moshi Magharibi katika jimbo la Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro.


Ni katika ziara iliyofanywa na mbunge wa jimbo hilo Prof Patrick Ndakidemi ambayo imelenga kuwapongeza kwa kuchaguliwa kwao kushika nafasi katika ngazi ya matawi, kata, Wilaya  na jumuiya za chama hicho. 


Mbunge huyo amewaasa kuimarisha  upendo na mshikamano baina yao na viongozi wa kisiasa na serikali sambamba na kuwaomba wazidi kuiunga mkono serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Samia Suluhu Hassan na kutetea kwa nguvu zote kazi kubwa zinazotekelezwa na serikali kutatua kero za wananchi wa Tanzania.


 Katika  mkutano huo, Mbunge amewaomba viongozi hao wawe mabalozi kwenye kuelezea umma kazi nzuri za maendeleo zinazotekelezwa na Serikali yao ya CCM iliyoko madarakani ambayo wameipigania.


Kwa upande wake diwani wa kata hiyo  Super Macha ameeleza miradi yote ambayo imetekelezwa na serikali tokea uchaguzi wa 2020 ulipokamilika na kuwa ni hatua kubwa katika kuleta maendeleo


Kwa mujibu wa diwani huyo miradi yenyewe ni pamoja na ule wa maji wa Tela Mande uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 905 na kufunguliwa rasmi ha Waziri Mkuu  Majaliwa Kassim Majaliwa. 


 Wajumbe wa mkutano huo wameonesha kuridhishwa kwa kiwango kikubwa kwa kazi kubwa ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi katika Kata ya Oldmoshi Magharibi. 


Pia wakaenda mbali zaidi na kuomba   wapatiwe nakala za ripoti hiyo ili wakawe mabalozi wa kuelezea uma kazi kubwa iliyofanywa na so ambapo diwani kwa kushiriana na mbunge wameahidi kuandaa na kuwapatia nakala hizo.


Baadhi ya kero ambazo zilizowasilishwa kwenye mkutano huo ni pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara kama ile ya Kiboriloni - Mande - Tela;  Mungureni - Mande; na Sango - Mandaka Mnono.


Halikadhalika kero ingine kubwa ni ile ya wafugaji kupeleka mifugo katika mashamba ya mpunga katika kijiji cha Mandaka Mnono na kulisha mifugo mazao yao jambo ambalo limekuwa likileta hasara kwa wakukima. 



Akijibu baadhi ya kero zilizowasilishwa  na baadhi ya wajumbe katika mkutano huo kwa niaba ya wananchi wa Oldmoshi Magharibi, Prof Ndakidemi  amesema kuwa kwa upande wa ubovu wa miundombinu ya barabara, ataendelea kulifanyia kazi kwa kushirikiana na diwani na viongozi wengine wa serikali  kama walivyofanya hapo awali kwenye baadhi ya maeneo korofi ambapo barabara zilitengenezwa, na makalavati kuwekwa kwenye sehemu korofi, na kudabua mito iliyokuwa inaharibu barabara.


 Amewahakikishia wajumbe kuwa kero zote ambazo zimewasilishwa atazitafutia ufumbuzi, kama alivyofanya kwenye utatuzi wa kero zingine hapo awali ambazo zilikuwa changamoto kubwa kwa wananchi. 


Ndakidemi amewashukuru  viongozi wote wa Chama cha Mapinduzi kata ya Oldmoshi Magharibi kwa kufanya naye kazi na diwani kwa ushirikiano, katika kuhakikisha wanatekeleza ilani ya chama hicho kwa vitendo, na kuhudumia wananchi ipasavyo kwa kuwatekelezea miradi mbalimbali ya maendeleo kama walivyo ahidi kipindi cha kampeni kwenye uchaguzi mkuu 2020.


Wakati wa kuhitimisha ziara ya Mbunge, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Oldmoshi Magharibi  Godson Mchau amempongeza mbunge kwa kutenga muda wake na kuja kusikiliza kero za wananchi ili zitafutiwe ufumbuzi

Share To:

Post A Comment: