Na,Jusline Marco;Arusha


Wakandarasi takribani 18 Mkoani Arusha wameingia makubaliano na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA kwa kutia saini mkataba wa ujenzi wa babarabara zilizopo katika jiji la Arusha.

Akiongoza zoezi la utiaji huo wa saini Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella 
amewataka wakandarasi waliopata tenda hizo kuwa wazalendo katika utekelezaji wa Miradi hiyo na kuwataka kuthibitisha ubora wa kazi zao,kupitia kazi watakazoenda kuzifanya ndani ya kipindi cha miezi 6 ili Wakazi wa mkoa wa Arusha waanze kunufaika na Miradi hiyo. 

Aidha Mongella amesema kukamilisha barabara hizo kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa  kutasaidia kushusha gharama za maisha kwa wananchi ambapo ameielekeza TARURA kusimamia wakandarasi hao kwa ukaribu zaidi ili wakamilishe miradi hiyo kwa wakati.

Mogella ameongeza kwa kumshukuru Rais Samia kwa kuongeza kiasi kikubwa cha fedha  katika miundombinu ya barabara Mkoa wa Arusha kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kutoka bilioni 9 hadi bilion 18.2 na kusema kuwa Rais hana deni kwenye barabara za mkoa wa  Arusha na kuboreshwa kwa miundombinu hiyo kutapunguza gharama za Usafiri.

Kwa upande Meneja wa Tarura mkoa wa Arusha mhandisi Laynas Sanya ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 walipatiwa jumla ya fedha za matengenezo ya barabara  ya zaidi ya bilioni 18 kwa awamu ya pili na katika awamu ya kwanza mikataba 34 ilisainiwa ikiwa na thamani ya bilioni 14 sawa na asilimia 60.

Ameongeza kuwa katika awamu ya pili ya utiaji saini katika mikataba 18 yenye thamani zaidi ya bilioni 4.07 sawa na asilimia 40 huku akisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 fedha walizopewa TARURA  katika bajeti yake zilizotokana na tozo za mafuta ili kusaidia katika ukarabati wa barabara katika Mkoa wa Arusha.      

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Missaile Musa amesema kuwa kitendo cha wakandarasi hao kusaini mikataba hiyo hadharani kutasaidia wananchi kuwafahamu wakandarasi watakaoenda kufanya kazi katika maeneo yao.

Nae Mkandarasi Rashidi Sevingi  kutoka kampuni ya Raly (EA) Limited amewahasa wakandarasi wengine kutekeleza mikataba waliyosaini kwa weledi ili waendelee kuaminiwa zaidi na Serikali.



Share To:

JUSLINE

Post A Comment: