Na John Walter-Manyara

 Maadhimisho ya siku ya wazee duniani yamefanyika hii leo, ambapo katika wilaya ya Babati mkoani Manyara maadhimisho hayo yamefanyika kwenye kituo cha kulelea wazee kilichopo katika kijiji cha Sarame wilayani Babati.

Katika maadhimisho hayo baadhi ya wazee wamepata nafasi ya kutoa maoni yao juu ya changamoto na mambo mbalimbali wanayopitia  na kuiomba serikali iwasaidie kutatua changamoto hizo. 

Baadhi ya changamoto zilizoelezwa na wazee hao ni suala la chakula kwani wamesema hawapati lishe bora itakayowasaidia kuwajenga kiafya.

Kwenye  suala la afya,Wazee wameiomba serikali iwasaidie kuwaletea karibu huduma za afya ili kuepuka usumbufu wa kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya.

Aidha wameishukuru serikali kwa kuwaletea huduma ya maji safi huku wakisema changamoto ni umbali katika kuyapata maji hayo.

Kwa upande wake afisa ustawi wa jamii wilaya ya Babati Mathias Focus ameeleza kuwa kwa sasa wanajitahidi kutoa huduma bora na za viwango kwa wazee kama lishe bora huduma za afya pamoja na maji, na kwamba changamoto zilizopo wanaendelea kuzifanyia kazi ili kutoa huduma bora kwa wazee.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amewaahidi wakazi wa kijiji cha sarame kuwa serikali itapeleka huduma za kijamii ambazo bado hazijafika kijijini hapo ikiwemo nishati ya umeme, maji na kuboresha miundombinu ya barabara ili ziweze kupitika kwa urahisi wakati wote.

Siku ya kimataifa ya wazeee huadhimishwa kila mwaka tarehe 1 mwezi Oktoba ambapo kwa mwaka huu maadhimisho hayo yanakwenda na kauli mbiu isemayo, “Ustahimilivu na mchango wa wazee, ni muhimu  kwa maendeleo ya taifa”.

Siku hii ilianzishwa mwaka 1990  baada ya mkutano mkuu wa umoja wa mataifa kuamua rasmi kuanzisha siku hii, na hadi sasa inakadiriwa kuwa kuna idadi ya wazee takribani milioni 703 wenye umri wa miaka 65 na kuendelea kwa mwaka 2019 lakini idadi hiyo inakadiriwa kuongezeka mara mbili zaidi kufikia mwaka 2050.

Hivyo kutokana na idadi ya wazee kuongezeka jamii zinaaswa kuishi vizuri na wazee na kuwasaidia pale inapohitajika kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.

Share To:

Post A Comment: