Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kuwezesha vijana wa kitanzania kusimamia na kuendesha mitambo ya kuchakata gesi nchini ambayo imewezesha gesi hiyo kusafirishwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo kwenye mitambo ya kuzalisha umeme, viwandani, majumbani na kwenye magari.

Pongezi hizo zimetolewa tarehe 11 Oktoba 2022, baada ya Wajumbe wa Kamati hiyo kufanya ziara katika visima vya gesi katika Kijiji cha Mnazi Bay na Msimbati pamoja na kiwanda cha kuchakata Gesi Asilia katika eneo la Madimba mkoani Mtwara. Ziara hiyo ililenga kujihakikishia kuwa shughuli za uzalishaji gesi pamoja na miundombinu yake inafanya kazi inavyostahiki.

“Kwa mfano kituo hiki cha Madimba ni muhimu sana kwa sekta yetu ya gesi nchini na kinaendeshwa na watanzania wenyewe katika mfumo mzima wa kuchakata gesi, Tunaipongeza Serikali kwa kuhakikisha kuwa maeneo kama haya yenye uwekezaji mkubwa yanaendeshwa na kumilikiwa na watanzania wenyewe.” Alisema Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Dunstan Kitandula

Alisema kuwa, gesi iliyopo inatumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo umeme ambapo zaidi ya asilimia 60 ya umeme nchini unazalishwa kwa kutumia Gesi Asilia na kuongeza kuwa, matumizi ya gesi yameongezeka hivyo ameiasa Serikali kuvutia uwekezaji zaidi na kuchimba gesi zaidi ili kukuza uchumi wa nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt.James Mataragio, alisema kuwa, mitambo ya kuchakata gesi ya Madimba inachakata gesi futi za ujazo milioni 210 kwa siku ambazo husambazwa kwa bomba kwenda maeneo mbalimbali ikiwemo ya viwanda, majumbani na kwenye mitambo ya umeme.

Alieleza kuwa, matumizi ya Gesi Asilia yanazidi kuongezeka hivyo Shirika hilo limejiandaa kuzalisha gesi zaidi ili kuweza kuwa na gesi ya kutosha kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: