OR -TAMISEMI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba wa kununuliwa kwa Mabasi mapya 177 Mwendokasi ya Wakala wa Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) jijini Dar es Salaam.


Bashungwa ameeleza hayo leo tarehe 03 Septemba 2022  alipoambatana na Kamati ya Kudumu ta Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kutembelea na kukagua miradi ya Wakala wa Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Dar es salaam.


Bashungwa ameeleza Ogezeko la mabasi hayo litawezesha DART kuongeza huduma kwa wananchi kutoka kuhudumia abiria 200,000 hadi kufikia 500,000 kwa siku katika vituo vyote vilivyopo sasa Dar es salaam.


"Mabasi ya mwendokasi yamepunguza kwa asilimia kubwa msongamano wa magari katika Mkoa wa Dar es Salaam na kuwawezesha wananchi kutumia muda mwingi kwenye kufanya kazi za uzalishaji pia kuwawezesha wanafunzi kufika mashuleni mapema bila adha kubwa za foleni," amesema Mhe.Bashungwa.


Aidha, Bashungwa amemuagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe kusimamia kikamilifu DART kufanya usanifu kwa haraka katika maeneo ambayo yapo pembezoni ili kuweka mpango wa kufikisha huduma ya Mabasi ya Mwendokasi, kama maeneo ya Vikindu, Kigambo, ukonga  na Chanika.


Waziri huyo amesema dhamira ya serikali ni kuongeza mtandao wa barabara za mwendokasi kwa kufikisha huduma ya mabasi katika maeneo pembezoni yenye watu wengi na kuboresha huduma katika maeneo ambayo yana huduma za mabasi ya mwendokasi.


Vile vile, Bashungwa amempongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupitisha muundo mpya wa kitaasisi wa Wakala huo ili kuwawezesha kutoa huduma ya usafiri kwa wananchi wa Dar es salaam.


Naye, Mwenyekiti wa Kamati PIC, Mhe. Jerry Silaa amepongeza DART  kwa kutumia mifumo ya TEHAMA katika utoaji huduma na kuwezesha mapato kuongezeka kutoka Sh.bilioni 25 hadi sh.bilioni 36 kwa mwaka wa fedha 2021/22.


Silaa ameitaka DART kurejea upembuzi yakinifu wa Mradi wa Mabasi yaendayo haraka uliofanyika mwaka 2004 ili kuwezesha kuweka mipango mipya ya kufikisha huduma katika maeneo ya pembezoni.


Pia amesema kuweka mpango wa kufikisha huduma katika Mikoa mingine kama Dodoma, Arusha, Mwanza na Mbeya.

Share To:

Post A Comment: