Na Fredy Mgunda, Iringa.


Hayo yamesemwa na viongozi waliotembelea TFS - Shamba la Miti SaoHill kwa ziara ya mafunzo kuanzia tarehe 02 hadi 03 Septemba kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma.


Katika ziara hiyo viongozi hao wamepata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazofanyika katika Shamba ikiwemo shughuli za uzalishaji miche na nyuki na maeneo ya viwanda vya uchakataji wa mazao ya misitu na nyuki.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kasulu , Kiongozi wa msafara Bw. Joseph Kashushura amesema kuwa ziara waliyoifaya imekuwa na manufaa makubwa kwani wameona namna shughuli mbalimbali za uhifadhi wa misitu zinavyofanyika na namna wananchi wanavyoshiriki katika  utunzaji wa rasilimali za misitu katika maeneo yao.


"Tumesafiri Mkurugenzi, Madiwani na wataalamu wachache kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu na TFS - Shamba la Miti Buhigwe - Makere kuja Shamba la Miti SaoHill ambalo lipo Mafinga kwaajili ya kujifunza jinsi ambavyo wanatunza misitu kama rasilimali" Bw. Joseph Kashushura, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu amesema.


Mkurugenzi amesema kuwa ni wakati umefika na wameona ni vyema kujifunza zaidi namna rasilimali za misitu zinavyosimamiwa katika maeneo mengine kama Shamba la Miti SaoHill ili wananchi katika maeneo yao wajifunze jinsi misitu inavyoleta faida za kiuchumi.


" Huko tunakotoka Kasulu tuna Shamba la Miti Buhigwe - Makere ambalo linasimamiwa na TFS lakini kumekuwa na muingiliano na wananchi ambao wanaingia kufanya shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo hivyo tumeona ni vyema madiwani waje waone ni kwa jinsi gani misitu inakuwa na manufaa kiuchumi na pindi watakaporejea wakawe mabalozi wazuri kwa wananchi wanaowasimamia", Mkurugenzi aliongeza.


Hata hivyo viongozi hao wamesema kuwa ushirikiano na elimu kubwa wanayopewa kuhusu uhifadhi wa misitu kuwa wananchi wanaozunguka misitu imekuwa ndio chachu kubwa kwa wananchi kutunza misitu katika maeneo yao Wilayani Mufindi na hivyo kupelekea misitu kuwa na faida kubwa kiuchumi  na kimazingira katika maeneo yao.


" Tumeona namna wenzetu wanavyotunza misitu na sisi tutaenda kuwaelimisha wananchi wetu faida kubwa za kiuchumi zinazopatikana katika misitu na pia tumeona namna elimu inavyotolewa ambayo inapelekea kujenga mahusiano mazuri baina ya wananchi wanaozunguka maeneo ya misitu kuhusu utunzaji wa maeneo ya hifadhi"  Alisema Bi. Agness Kanyamagenge, Diwani Viti maalumu Kasulu DC


Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kasulu amesema kuwa wamefurahia ziara hii ambayo imeandaliwa na TFS kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ili kupata elimu zaidi kuhusu uhifadhi wa misitu katika maeneo yao na faida mbalimbali kiuchumi na kimazingira zinazopatikana kutoka na uwepo wa misitu kama ilivyo katika Wilaya ya Mufindi ambapo Halmashauri zake zinafaidika na tozo mbalimbali zinazopatikana kutokana na mazao yatokanayo na misitu.


Akiwasilisha taarifa ya Shamba Msaidizi wa Mhifadhi Mkuu - Mipango na Matumizi Ignas Lupala kwa niaba ya Mhifadhi Mkuu amesema kuwa katika uhifadhi wa misitu suala la uelewa wa pamoja kuhusu utunzaji wa misitu ni jambo la muhimu na hivyo aliwaeleza kuwa elimu watakayoipata ni vyema kuwashirikisha wananchi namna uhifadhi wa misitu ilivyo na faida kubwa kiuchumi na kimazingira.


Naye Askari Mhifadhi kutoka TFS - Shamba la Miti Buhigwe - Makere Rodgers Kaijunga amesema kuwa wataendeleea kutoka elimu na kuwahamasisha wananchi kuhusu masuala ya uhifadhi wa misitu na faida zake kiuchumi na kimazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho na kuendelea kuwaahidi wananchi ushirikiano katika masuala ya uhifadhi wa misitu.

Share To:

Post A Comment: